Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 09Article 541804

Habari Kuu of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tamisemi yajitosa kudhibiti mikopo makundi maalumu

Tamisemi yajitosa kudhibiti mikopo makundi maalumu Tamisemi yajitosa kudhibiti mikopo makundi maalumu

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imesema itahakikisha utekelezaji wa utoaji na urejeshaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri wanayopewa wanawake, vijana na wenye ulemavu katika halmashauri zote.

Naibu Waziri wa Nchi, Tamisemi, Dk Festo Ndugange, alibainisha hayo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Maswa Mashariki, Staslaus Nyongo (CCM).

Katika swali lake, Nyongo alisema hali ya urejeshi wa mikopo inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu si ya kuridhisha, hivyo alitaka kujua mkakati wa serikali kuhakikisha urejeshaji wa fedha hizo unafanyika sawia.

Akijibu swali hilo, Dk Ndugange alikiri kusuasua kwa urejeshaji wa fedha hizo kwa baadhi ya vikundi vilivyokopeshwa.

"Ni kweli fedha hizo za asilimia 10 zimewekwa kisheria ili ziwe zinazunguka kwa kutekeleza shughuli za wajasiriamali na kuzirejesha bila riba yoyote ili fedha zile ziweze kutumika kuwakopesha wengine, lakini hata hivyo, kumekuwa na changamoto ya urejeshaji wa fedha hizo kwa baadhi ya vikundi vya wajasiriamali na tunakwenda kufungua akaunti ili kuhakikisha kila kikundi kinarejesha fedha walizochukua," alisema.

Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia suala la mikopo hiyo na urejeshaji wake ili fedha hizo zikopeshwe kwa vikundi vingine.

"Ofisi ya Rais-Tamisemi tunakwenda kufanya ukaguzi ili kuona fedha zinarejeshwa na zinakopeshwa katika vikundi vingine," alisema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Mwantum Day Haji (CCM), alitaka kujua ni lini serikali itaanza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana katika halmashauri wanakopewa mikopo hiyo.

Akijibu swali hilo, Dk Ndugange alisema kwa mwaka 2019/2020 mamlaka za serikali za mitaa zimetoa mafunzo kwa vikundi 11,915.

"Kwa mujibu wa Kanuni ya 23 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya Asimilia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za Mwaka 2019, mamlaka za serikali za mitaa zinapaswa kutoa mafunzo kwa vikundi vilivyokubaliwa kupata mikopo hiyo.

"Kwa kuzingatia kanuni hiyo, serikali ilikwishaanza kutoa elimu ya ujasiriamali na katika mwaka wa fedha 2019/20, mamlaka za serikali za mitaa zimetoa mafunzo kwa vikundi 11,915 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambavyo vilipewa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,” alisema.

Kwa mujibu wa Ndugange, mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na ya ujasiriamali, utunzaji fedha, uendeshaji na usimamizi wa miradi, utoaji taarifa na usimamizi wa marejesho ya mikopo.

Join our Newsletter