Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542203

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania, Botswana kuimarisha biashara

RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais na Rais wa Botswana Dk Mokgweetsi Masisi wamekubaliana nchi zao ziimarishe ushirikiano katika maeneo mbalimbali yakiwemo biashara na uwekezaji.

Viongozi hao pia wamewataka mawaziri wa mambo ya nje wa Tanzania na Botswana waifufue Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) iliyoanzishwa mwaka 2002 na waanze kukutana ndani ya miezi mitatu.

Walitoa maagizo hayo jana Ikulu Dar es Salaam baada ya kuzungumza kuhusu masuala yanayohusu nchi hizo.

Rais Samia alisema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Botswana ni kidogo kwa kuwa mwaka 2005 thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili kilikuwa Sh milioni 731 za Tanzania na hadi kufikia mwaka jana kilifikia Sh bilioni 3.5.

“Tumekubaliana tuwahamasishe wafanyabishara wetu kutumia fursa za kibiashara zilizopo ili kukuza kiwango cha biashara kwani bado ni kidogo,”alisema.

Rais Samia alisema Botswana imewekeza nchini miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 231 iliyotoa ajira 2,128 kwa Watanzania na kwamba, moja ya miradi hiyo ni wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Alitaja eneo lingine la ushirikiano walilolipa kipaumbele ni mifugo, nyama na madini.

Samia alisema Botswana inaongoza kwa kuuza nyama nje ya nchi ikilinganishwa na Tanzania, hivyo

kuna haja ya wataalamu wa nchi hizo mbili kubadilishana uzoefu katika eneo hili.

Kuhusu madini alisema Botswana inaongoza duniani kwa kuuza madini ya almasi hivyo Tanzania itatuma wataalamu waende Botswana kujifunza mikakati na namna bora ya kuweza kuvuna rasilimali hiyo nchini kwa faida ya Watanzania.

Pia alisema walikubaliana kukuza ushirikiano wa kikanda, kibara na kidunia kupitia Jumuiya walizomo ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa

Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).

Rais Masisi alisema wamewataja mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo mbili kuhakikisha wanaifufua Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na waanze kukutana ndani ya miezi mitatu.

“Tumewataka waainishe maeneo ya ushirikiano tuliyokubaliana ikiwemo utalii, mifugo, ulinzi na usalama, uzalishaji wa dawa na Covid-19, uzalishaji wa kilimo, michezo, mazingira, elimu na siasa,”alisema.

Rais Masisi pia alimpongeza Samia kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika SADC na alimualika aende Botswana. Rais Samia ameukubali mwaliko huo.

Aidha, Rais Samia na Rais Masisi walishuhudia kusainiwa kwa tamko la pamoja la nchi zao uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana, Dk Lemogang Kwape.

Join our Newsletter