Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 26Article 553747

Habari Kuu of Thursday, 26 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania, Kenya zakubaliana diplomasia, elimu, mipaka

Tanzania, Kenya zakubaliana diplomasia, elimu, mipaka Tanzania, Kenya zakubaliana diplomasia, elimu, mipaka

TANZANIA na Kenya zimesaini hati tatu za makubaliano ya ushirikiano kwenye kushauriana kisiasa na kidiplomasia; uhakiki wa mpaka kati yao na hati ya makubaliano ya ushirikiano katika elimu ya juu, sayansi na teknolojia.

Viongozi wa nchi hizo walisaini makubaliano hayo jijini Nairobi wakati wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Raychelle Omamo waliongoza mkutano huo uliohudhuriwa pia na mawaziri, makatibu wakuu na maofisa waandamizi kutoka Tanzania na Kenya.

Mkutano huo ulifanyika kutekeleza ya maagizo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta walipokutana wakati wa ziara ya Rais Samia nchini humo Mei mwaka huu.

Mawaziri wa Tanzania waliohudhuria ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi; wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wa Madini, Dotto Biteko, na wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Khalid Salum Mohammed, na naibu mawaziri Khamis Chilo (Mambo ya Ndani ya Nchi), na Exaud Kigahe (Viwanda na Biashara).

Balozi Mulamula alisema mkutano huo ni hatua muhimu kwenye uhusiano kati ya nchi na nchi na kwamba ana imani yaliyokubalika yatatekelezwa kwa ufanisi.

Alisema hati ya makubaliano kuhusu uhakiki wa mpaka yatatoa msingi wa kisheria wa kuhakiki mpaka uliowekwa na wakoloni kwa kuuimarisha na kuweka alama zinazoonekana ili kuondoa mwingiliano wa jamii za mpakani na hivyo kupunguza migogoro ya mara kwa mara.

Balozi Mulamula alisema hati ya ushirikiano kwenye masuala ya elimu inalenga kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote katika maeneo ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia ili kuleta manufaa kwa nchi zote katika kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa masuala ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia kwa pande zote.

Alisema hati ya ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia ina umuhimu katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano mzuri wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Kenya na katika ngazi za kikanda na kimataifa.

Balozi Omamo aliishukuru Tanzania kwa kushiriki na kwa kuupa uzito mkutano huo na kwamba hiyo inaonesha nia iliyopo ya kukuza ushirikiano wa kihistoria na kindugu kati ya Kenya na Tanzania.

Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ilianzishwa Septemba 2009 jijini Arusha na Mkutano wa Kwanza ulifanyika jijini humo mwaka huohuo.

Mkutano wa Pili ulifanyika Nairobi, Septemba 2012 na wa Tatu ulifanyika Dar es Salaam Desemba 2016.