Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 24Article 573823

Habari Kuu of Wednesday, 24 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Tanzania ina uwezo wa kuzalisha megawati 5000 umeme jotoardhi

Tanzania ina uwezo kuzalisha Megawati 5000 umeme wa jotoardhi Tanzania ina uwezo kuzalisha Megawati 5000 umeme wa jotoardhi

Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imesema kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 5000 za umeme (MWe) zitokanazo na jotoardhi.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Meneja Mkuu na Mtendaji Mkuu wa TGDC, Kato Kabaka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Amesema jotoardhi hilo ambalo linatokana na joto la asili la dunia lililopo chini ya ardhi katika mfumo wa majimoto, mvuke au miamba mikavu linapatikana katika mikoa zaidi ya 16 ya Tanzania bara.

Kabaka amesema maeneo hayo yapo katika sehemu zilizopitiwa na Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki na Magharibi na kuongeza kuwa kulingana na mpango wa Taifa wa uzalishaji umeme wa mwaka 2020 wanalengo la kuzalisha Megawati 200 na 500 za joto zitokanazo na jotoardhi ifikapo mwaka 2025.

Amesema jotoardhi linafanya kazi ya kuzalisha umeme pamoja na joto ambalo husukuma na kuzungusha mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme nchini.

Hata hivyo amesema katika kipindi cha miaka 60 wamefanikiwa kutoa mafunzo katika nyanja hiyo ya jotoardhi kwa wataalamu wapatao 30 kutoka saba ngazi ya stashahada na umahiri.

“Mafunzo ya jotoardhi hayatolewi na vyuo vya ndani ya nchi bali utolewa na vyuo vya nje, mpaka sasa tumewezesha wataalamu hao kwenda kusoma na wengine bado wapo nje ya nchi wakikamlisha kozi zao,” amesema

Amesema ili kutumia jotoardhi katika kuchochea ukuaji wa sekta jingine mbali na umeme, TGDC inaendelea na mradi wa kuzalisha kuku, kilimo cha mbogamboga na ufugaji samaki katika eneo la majimoto Songwe.

“Lengo la miradi hii ni kuonesha jinsi rasilimali ya jotoardhi inavyoweza kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi na kutoa fursa za ajira mpya kwa vijana,” amesema

Pia amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya Megawati 15,000 za joto kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja ya jotoardhi.