Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 10Article 542044

Habari Kuu of Thursday, 10 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania kuongoza mkutano Baraza Kuu UN

Tanzania kuongoza mkutano Baraza Kuu UN Tanzania kuongoza mkutano Baraza Kuu UN

TANZANIA imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 76) katika uchaguzi uliofanyika Juni 7 mwaka huu mjini New York nchini Marekani.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Buhohela alisema katika uchaguzi huo, Tanzania ilipita bila kupingwa na mara ya mwisho Tanzania kuwa Makamu wa Rais ni 1991.

“Majukumu ya Makamu

wa Rais ni kusaidiana na Rais katika kuratibu na kusimamia shughuli za mijadala ya UNGA na kamati zake katika kutunga maazimio. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ndiyo chombo kikuu cha kutunga sera na sheria chenye uwakilishi wa nchi zote wanachama ambapo mkutano wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika mwezi Septemba,”alisema Buhohela.

Kwa mujibu wa Buhohela, Tanzania iliwahi kuwa Rais wa UNGA mwaka 1979 katika mkutano wa 34 wakati wa uwakilishi wa Balozi Dk Salim Ahmed Salim.

Pia alisema katika uchaguzi huo Tanzania imeshinda nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Uchumi na Jamii la

Umoja wa Mataifa (ECOSOC) kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Januari Mosi mwakani hadi Desemba 31 mwaka 2024 ambapo katika uchaguzi huo Tanzania ilipata kura 182 kati ya kura 186 zilizopigwa na nchi wanachama 54 zinazounda umoja huo.

“Hii ni mara ya tano kwa Tanzania kushika nafasi hii ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1966-1969 na kufuatiwa mwaka 19781980, 1994-1996 na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2004-2006,” alisema Buhohela.

Alisema ECOSOC ndicho chombo kinachohusika na miradi ya maendeleo ya kiuchumi ya UN hasa katika kutekeleza Malengo

ya Maendeleo Endelevu ya 2030 pamoja na kusimamia mashirika yaliyo chini ya UN kama vile UNDP, UNFPA na UNICEF.

Buhohela alisema kuchaguliwa kwa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni ishara ya kuaminika katika medani za kimataifa na nchi wanachama wa UN.

Kwa nafasi ya Rais wa umoja huo, alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Maldives, Abdulla Shahid ndiye aliyechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kura 143 dhidi ya mpinzani wake ambaye ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, Dk Zalmai Rassoul aliyepata kura 48.

Join our Newsletter