Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 23Article 559318

Habari Kuu of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania kupokea shehena nyingine chanjo ya COVID-19

Tanzania kupokea shehena nyingine chanjo ya COVID-19 Tanzania kupokea shehena nyingine chanjo ya COVID-19

WIZARA ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajiwa kupokea shehena nyingine ya chanjo ya Covid 19 mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza katika mkutano wa majadiliano baina ya serikali na vyombo vya habari yaliyoandaliwa na Mradi wa Boresha Habari unaodhamiwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na kutekelezwa na Internews, Afisa Habari wa Wizara ya Afya, Said Makora, amesema lengo la serikali ni ni kuhakikisha angalau asilimia 60 ya wananchi wake kupata chanjo hiyo ya Corona.

Julai, mwaka huu, Tanzania ilipokea dozi 1,058,400 za chanjo aina ya Johnson & Johnson kutoka Marekani ikiwa sehemu ya ahadi ya taifa hilo lenye nguvu za kiuchumi zaidi duniani ya kutoa angalau dozi milioni 25 kwa Afrika kati ya dozi milioni 80 zilizoahidiwa kwa bara hilo kupitia mpango wa ‘Covax Facility’ ambao Tanzania ni miongozi mwa nchi zilizojiunga na mpango huo.

Mpango wa Covax unalenga kuhakikisha nchi masikini kote duniani zinapata mgao sawa wa chanjo licha ya ufinyu wa uwezo wao wa kiuchumi. Unaundwa chini ya mwavuli wa mashirika mbalimbali ikiwemo Shirika la Afya Duniani na baadhi ya serikali za nchi tajiri duniani.

idha Makora amesema ili kufikia lengo la asilimia 60 ya wananchi kupata chanjo, Wizara ya Afya wiki iliyopita imezindua Mpango wa Jamii Shirikishi na Harakishi wa Chanjo ya COVID19 (Mobile Vaccination Site) na kuwafuata Wananchi walio tayari kuchanjwa.

Makora amesema mpango huo unalenga kuongeza vituo vya kuchanja kutoka 550 hadi 6,784 ili kuharakisha Wananchi kuchanjwa mapema na wiki ijayo Mikoa itaweka wazi mwenendo wa uhamasishaji na uharakishaji wa kutoa huduma za Chanjo ya Corona.

Amesema pia mpango huo utasimamiwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa na kwamba wiki ijayo Mikoa na Wilaya na wadau wengine wakiwemo WHO, Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Chuo Kiku cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) na wadau wengine tayari wamekubaliana na kuweka mkakati wa utekelezaji wa mpango wa kutoa habari sahihi kwa Umma kuhusu Chanjo ya Covid 19 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Kwa upande wa Mkufunzi Mwandamizi wa Internews, Alakok Mayombo, amesema kuwa uwazi na uwajibikaji ni mambo muhimu katika zoezi hilo, kwani nchi inafanya mpango wa uhamasishaji wa chanjo katika ngazi zote za mkoa na wilaya.

Mayombo amesema Internews kwa sasa inawasaidia waandishi wa habari na vituo vya habari vya jamii kufikia makudni tofauti kwa kuwapa habari sahihi juu ya Covid-19 na chanjo.

Wiki iliyopita, serikali ilizindua programu inayojumuisha na inayofuatilia kwa haraka jamii ambayo iliongeza idadi ya vituo vya chanjo ya Covid-19 kutoka 550 hadi 6,784, makadirio ya kumaliza akiba ya chanjo zilizobaki kwa muda wa wiki mbili.

Mpango huo ulizinduliwa katika mji mkuu wa nchi ya Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Doroth Gwajima.

Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Abel Makubi alisema umma haupaswi kulaumiwa kwa kusita kuchukua chanjo, akisema wataalam wa afya lazima wafanye kazi yao vizuri kwa kuwaelimisha juu ya athari chanjo za chanjo.