Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 19Article 552331

Habari Kuu of Thursday, 19 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania kuwa kitovu kukabili ugaidi SADC

Tanzania kuwa kitovu kukabili ugaidi SADC Tanzania kuwa kitovu kukabili ugaidi SADC

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera amesema uamuzi wa wakuu wa nchi na serikali za jumuiya hiyo kuichagua Tanzania kuwa kituo cha kukabiliana na ugaidi ni sahihi.

Alisema hayo jana wakati akifunga mkutano wa 41 wa wakuu hao mjini Lilongwe, nchini Malawi.

Mkutano huo ulikuwa wa siku mbili kuanzia Agosti 17 hadi jana.

Rais Chakwera alisema ni nadra kukosekana kwa utulivu na ukosefu wa usalama katika ukanda wa SADC na inapotokea hivyo suala hilo linashughulikiwa kwa ukamilifu kupitia Ogani ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama.

“Kituo hiki kitakuwa ni kielelezo kingine cha azimio letu la kutotoa nafasi kwa ugaidi na misimamo mikali na kuifanya jamii yetu kuwa na amani,” alisema.

Dk Chakwera alisema hakuna sehemu nzuri duniani ambako mambo kama hayo yanaweza kufanyika zaidi ya SADC kwa sababu eneo hilo lina amani, usalama na utulivu.

Katika hatua nyingine, kwa kuzingatia kuwa kaulimbiu ya mkutano huo kwa mwaka huu ilikuwa ‘Kuimarisha uwezo wa uzalishaji katikati ya janga la covid-19 kwa mabadiliko endelevu ya kiuchumi na viwanda,’ Rais Chakwera alisema huo ni mwito kwa nchi zote wanachama wa SADC kuitikia kwa vitendo na bidii katika kukabiliana na athari za ugonjwa huo kijamii na kiuchumi.

“Huu ni wakati wa SADC kujijenga upya na kubadilisha rasilimali zake za uzalishaji, pia ni wakati wa kuwezesha uwezo wa kijasiriamali wa watu wake pamoja na kuanzisha uhusiano wa uzalishaji kwa ajili ya kufanikisha mabadiliko ya kimuundo na viwanda.”

“Sasa ni wakati wetu wa kuifanya SADC tunayoitaka iwe tunayoifurahia. Aina ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi tunayofikiria hayawezi kupatikana bila ya mapinduzi ya viwanda, kuhama kutoka malighafi na vitu visivyosindikwa kwenda kwenye bidhaa zilizoongezwa thamani ni jambo la lazima na Mkakati na Mpango wa Viwanda wa SADC, ni muhimu katika kufanikisha hili,” alisema.

Rais Chakwera alisema jambo jingine la msingi ni mapinduzi ya kidijitali ambayo ni hitaji muhimu katika zama hizi za covid-19.

Alitoa mwito wa kuimarisha eneo la kidijiti katika SADC kwa ajili ya biashara mtandao na utoaji huduma za kitabibu kwa mtandao.

Alisema hakunabudi kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji wa itifaki za SADC zinazohusu usafirishaji, mawasiliano na metrolojia pamoja na Azimio la SADC la Mwaka 2001 Kuhusu Habari, Mawasiliano na Teknolojia.

Katibu Mtendaji aliyemaliza muda wake, Dk Stergomena Tax alisema baadhi ya mambo ambayo wakuu wa nchi na serikali wa SADC waliyafanya kwenye mkutano huo ni pamoja na kumchagua Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kuwa Mwenyekiti wa Ogani ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya jumuiya hiyo.

Alisema mengine ni kuthibitisha uteuzi wa Katibu Mtendaji mpya wa SADC, Elias Magosi raia wa Botswana, kumpongeza Dk Taxi kwa kuitumikia SADC kitaalamu, kwa umakini, pamoja na kuidhinisha mabadiliko ya Jukwaa la Bunge la SADC kuwa Bunge la SADC kama chombo cha kushauriana na kujadiliana.

Wakati wa kilele cha mkutano huo jana, wakuu wa nchi na serikali walishuhudia Jaji Mkuu wa Malawi, Andrew Nyirenda akimwapisha Katibu Mtendaji mpya wa SADC, Magosi.