Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 29Article 544630

Habari Kuu of Tuesday, 29 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania kuweka historia umeme EAC, SADC

Tanzania kuweka historia umeme EAC, SADC Tanzania kuweka historia umeme EAC, SADC

WIZARA ya Nishati imesema ubunifu na weledi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya nishati utaiwezesha Tanzania kuingia katika historia Afrika Mashariki (EAC) na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuzalisha umeme mwingi.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Medard Kalemani aliyasema hayo Dar es Salaam wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwenye kipindi kuhusu siku 100 za Rais Samia madarakani.

Rais Samia aliapishwa Machi 19 mwaka huu baada ya kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli. Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Dk Kalemani alimpongeza Rais Samia kwa kuweka nguvu kwenye nishati na kwamba katika mwaka wa fedhaa 2021/2022 sekta hiyo imepatiwa Sh trilioni 2.835. Katika mwaka wa fedha unaokwisha ilitengewa Sh trilioni 1.97.

“Hatunabudi kumpongeza kwa kuwa ameona tunakwenda kujenga uchumi wa viwanda na njia pekee ya kutuwezesha kufika huko kama Watanzania ni kupitia nishati ya umeme. Na hatua ya kwanza ya uwezeshaji ni upatikanaji wa nishati ya umeme,” alisema.

Dk Kalemani alisema kwa sasa Tanzania inazalisha umeme megawati 1,604.24 unaotumika kwa matumizi mbalimbali. Alisema asilimia 68 ya umeme huo unazalishwa kwa gesi ambayo ni takribani megawati 901 na kiasi kilichobaki kwa kiasi kikubwa ni rasilimali ya maji.

Dk Kalemani alisema matumizi ya juu kabisa ni megawati 1,208 hadi 1,280 hivyo kuna ziada ya megawati 92. Alisema Rais Samia aliielekeza wizara hiyo itekeleze miradi mikubwa ya kimkakati ili nchi itoke kwenye changamoto za nishati.

Dk Kalemani alisema serikali inatekeleza miradi kadhaa ya umeme ukiwemo wa bwala la Nyerere unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115.

Alisema pia kuna miradi mingine ukiwemo wa Malagarasi na kwamba, yote ikikamilika nchi itakuwa inazalisha megawati za umeme 4,800 na kwa mujibu wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) lengo ni kufikisha megawati 5,000 ifikapo mwaka 2025.

Kuhusu umeme vijijini, Dk Kalemani alisema katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya Sh trilioni 1.24 zimetengwa kwa ajili ya kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobaki.

“Nchi ina jumla ya vijiji 12,268 na hadi sasa umeme umeshapelekwa katika vijiji 10,361 bado takribani vijiji 9,100 katika nchi za Afrika kwa sasa nchi yetu inaongoza,” alisema na kusema katika siku 100 za Rais samia umeme umepelekwa katika vijiji 400.