Uko hapa: NyumbaniInfos2019 11 10Article 487330

General News of Sunday, 10 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Bodi ya Mikopo yatenga Sh1.8 bilioni kwa wanafunzi watakaoshinda rufaa

Bodi ya Mikopo yatenga Sh1.8 bilioni kwa wanafunzi watakaoshinda rufaa

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetenga Sh1.8 bilioni kwa ajili ya wahitaji wa mikopo watakaokata rufaa baada ya dirisha la rufaa kufunguliwa Novemba 10, 2019.

Hadi sasa, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo wa 2019/2020 wapatao 46,838 wamepata mikopo yenye thamani ya Sh162.86 bilioni.

Bodi inasema jumla ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wote ni Sh450 bilioni na kati ya hizo, Sh164.6 bilioni ni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza pekee na Sh285.4 bilioni watakopeshwa wanafunzi wanaoendelea na masomo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa HESLB, Abdul Razaq Badru alisema ufunguaji wa dirisha hilo una lengo la kuwapatia fursa wanafunzi wenye uhitaji ambao walikosa mikopo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kukosea kujaza fomu na wengine hawakuambatanisha nyaraka muhimu.

Alizitaja nyaraka hizo ni vyeti vya vifo vya wazazi kwa wale waliofiwa na mzazi mmoja ama wote wawili, barua za udhamini kwa waliodhaminiwa na uthibitisho wa udahili.

“Sh1.8 bilioni zipo na kwa waombaji wa mikopo, fedha siyo tatizo ni wao kuthibitisha uhitaji wao,” alisema Badru.

Alisema bodi tayari imeshatoa taarifa ya kufunguliwa kwa dirisha hilo mapema, lengo likiwa ni kutoa muda kwa waombaji kukusanya nyaraka ambazo awali hawakuziambatanisha.

“Waombaji watapaswa kujaza fomu mtandaoni wakiambatanisha na nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, hadi kufikia Novemba 25 tutakuwa na orodha kamili ya wanafunzi wote ambao rufani zao zitakuwa zimeshinda,” alisema mkurugenzi huyo.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kwenda sambamba na msimu wa ufunguaji wa vyuo vyote nchini.

Dk Veronica Nyahende, meneja uchambuzi na upangaji mikopo wa HESLB alisema fedha hizo ni mkopo, hivyo wanasisitiza uambatanishaji wa nyaraka ni muhimu kwa sababu kutaisaidia Serikali kukusanya madeni yake kutoka kwa wakopaji.

“Lengo letu ni kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye uhitaji aliyeomba mkopo anapata fedha. Pia wale 5,000 ambao walipewa ruhusa ya kurekebisha taarifa zao dirisha bado lipo wazi, waendelee kufanya hivyo,” alisema Dk Nyahende.

Katika kipindi cha miaka minne, bodi hiyo imekuwa ikiongezewa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi hao wa elimu ya juu. Mwaka 2014/15 zilitengwa Sh341 bilioni na hadi mwaka 2019/2020, zimefikia Sh450 bilioni.

Mbali na ongezeko la fedha hizo, pia kumekuwa na ongezeko la wanufaika, mwaka 2014/2015 walikuwa wanafunzi 100,936, mwaka 2019/2020 wameongezeka na kufikia 128,285.

Kwa mujibu wa Badru, mbali na mafanikio hayo, katika kipindi cha miaka minne makusanyo ya mikopo hiyo yameongezeka kutoka Sh21.16 bilioni mwaka 2014/2015 na kufikia Sh183 bilioni mwaka 2018/2019.

Join our Newsletter