Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540442

Habari Kuu of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania ya 13 kuchangia walinzi wa amani

Tanzania ya 13 kuchangia walinzi wa amani Tanzania ya 13 kuchangia walinzi wa amani

TANZANIA imetajwa kuwa nchi ya 13 duniani kwa kuchangia kwa wingi askari vikosi kwenye Umoja wa Mataifa (UN).

Nafasi hiyo ni miongoni mwa nchi 122 duniani huku kwa upande wa nchi 35 za Afrika zinazochangia askari katika vikosi hivyo, ikishika nafasi ya saba.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alisema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Walinzi wa Amani, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Mbarouk aliihakikisha UN kuwa iko tayari wakati wowote kuendelea kutoa vikosi vya askari wake kwenda kushiriki katika misheni za ulinzi wa amani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mbarouk , tangu Tanzania ianze kupeleka vikosi hivyo katika misheni za ulinzi wa amani za UN, askari wake 1,481 wameshiriki katika takribani misheni sita za ulinzi wa amani.

Alitaja nchi ambazo askari hao walipelekwa kwa ajili ya misheni hizo kuwa ni Sudan Kusini, Sudan, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Afrika ya Kati na Lebanon.

“Pamoja na kutambua mchango wetu kwenye misheni za ulinzi wa amani kupitia maadhimisho haya, vilevile tunajumuika siku hii ya leo (jana) kwa lengo la kuungana na nchi zingine wanachama wa UN ili kuwakumbuka walinda amani wote waliopoteza maisha,” alisema.

Alisema tangu kuanzishwa kwa misheni za kulinda amani mwaka 1948, Umoja wa Mataifa umepoteza zaidi ya walinda amani 4,000 kwenye operesheni zilizofanywa maeneo mbalimbali duniani na kati yao walinda amani 60 walikuwa ni Watanzania.

Awali, Ofisa Kiongozi Ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Helge Flard alisema maadhimisho ya siku hiyo yamelenga kuwakumbuka walinda amani 4,000 waliopoteza maisha wakiwa katika misheni na kuwapa moyo zaidi ya walinda amani milioni moja walioko kwenye misheni hizo.

Stella Vuzo kutoka Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa Tanzania, alisema misheni za walinda amani zilianzishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusaidia pale panapotokea machafuko na walinda amani hao hutolewa na nchi wanachama wa UN.

Katibu Mkuu wa UN, António Guterres akiwa Makao Makuu ya UN, Washington, Marekani, katika kuadhimisha siku hiyo ya walinda amani, aliweka mashada ya maua katika mnara wa kumbukumbu ya askari 4,000 waliopoteza maisha kwenye misheni za amani.

Alitoa nishati kwa askari wa ulinzi wa amani wakiwemo wanajeshi, polisi na raia 129 waliopoteza maisha yao katika misheni za ulinzi wa amani mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu wakiwamo Watanzania wawili; Sajeni Adson Mwinyi Kombo aliyekuwa kwenye misheni DRC na Inspekta Bernard Kapusi aliyekuwa kwenye misheni Sudan Kusini.

Join our Newsletter