Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 06Article 561619

Habari Kuu of Wednesday, 6 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania yapata bil 196/- kuimarisha elimu

Tanzania yapata bil 196/- kuimarisha elimu Tanzania yapata bil 196/- kuimarisha elimu

SERIKALI ya Tanzania imesaini mkataba na Serikali ya Sweden wa kupokea fedha za msaada Krona milioni 750 za Sweden sawa na Sh bilioni 195.9 kwa ajili ya awamu ya pili ya Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EP4R II).

Mkataba huo kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na kwa upande wa Sweden ulisainiwa na Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjöberg, Dar es Salaam jana.

Tutuba alisema Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EP4R) awamu ya pili utatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia Julai mwaka huu hadi Juni mwaka 2026 kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu msingi.

“Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (SIDA), imechangia takriban shilingi bilioni 207.7 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mpango huu. Natoa shukrani zangu za dhati kwako binafsi na kupitia wewe Serikali ya Sweden kwa ajili ya mchango wa awamu iliyopita na ahadi ya leo,” alisema Tutuba.

Alisema Agosti 26, mwaka huu, Serikali ya Tanzania na Sweden zilisaini mkataba wa msaada wa SEK milioni 450 sawa na Sh bilioni 117.6 kwa ajili ya Mpango wa Pili wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN II), hivyo EP4R II inachukua nafasi ya awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 2014/2015 na kuishia mwaka 2019/2020 ambapo SIDA na Benki ya Dunia ziliongeza muda na ufadhili hadi 2020/2021.

Kwa mujibu wa Tutuba, Mpango wa Elimu kwa Matokeo unachangiwa na wafadhili mbalimbali wakiwemo FCDO, Benki ya Dunia, SIDA, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA) na Shirika la Elimu Duniani (GPE) kwa kutumia mfumo wa mpango kwa matokeo kuleta mabadiliko yenye tija katika sekta ya elimu msingi Tanzania.

Aliyataja baadhi ya mafanikio ya Mpango wa Elimu kwa Matokeo Awamu ya Kwanza kutoka mwaka 2014/2015 hadi 2020/2021 kuwa ni ujenzi wa madarasa 10,409, vyoo 20,507, mabweni 646, nyumba za walimu 91, majengo ya utawala 37, maktaba 49, maabara 29, uzio katika shule tatu na uchimbaji wa visima vya maji katika shule 16.

Mafanikio mengine ni ujenzi wa ofisi 155 za uthibiti wa ubora wa shule na kuweka vifaa na kuboresha mazingira ya kazi na kusogeza karibu huduma kwa wateja wa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa shule mpya 44 kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi, ukarabati wa shule kongwe za serikali 86 na ukarabati wa ofisi 31 za uthibti wa ubora wa shule.

Balozi Sjöberg alisema lengo kuu la SIDA ni kutengeneza fursa kwa watu wanoishi kwenye umaskini na ukandamizaji ili kuboresha maisha yao, hivyo kwa Tanzania elimu ni moja ya malengo muhimu katika mkakati wa Sweden.

Alisema Tanzania na Sweden zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya elimu tangu Uhuru na mchango wao kwenye sekta hiyo umekuwa wa uwekezaji mkubwa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo alisema msaada huo wa fedha utasaidia upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa Tanzania na kuongeza kuwa uhusiano wa Tanzania na Sweden ulianza tangu mwaka 1961 na sasa unatimiza miaka 60.