Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 31Article 554536

Habari Kuu of Tuesday, 31 August 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Tanzia: DCI Manumba Afariki Dunia

Tanzia: DCI Manumba Afariki Dunia Tanzia: DCI Manumba Afariki Dunia

MKURUGENZI Mstaafu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini (DCI) Robert Manumba amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne, Agosti 31, 2021 katika hospitali ya taifa Muhimbili alipokua akipatiwa matibabu.

Mwanaye, Rose Manumba amethibitisha kutokea kwa msiba huo na kuandika haya kupitia Twitter; Baba yangu Robert Manumba, ahsante kwa kunionyesha maana halisi ya upendo wa Baba kwa mtoto na kuamini katika juhudi zangu kuwa naweza kuwa bora katika chochote kile nachotaka. Tulicheka pamoja na tulilia pamoja. Nitakupenda milele. Mwenyezi Mungu akupumzishe kwa Amani baba yangu.”

Manumba ambaye alistaafu mwaka 2013, katika utumishi wake, amelitumikia jeshi hilo katika nyadhifa mbalimbali zikiwamo katika Chumba cha Kupokea Mashtaka kati ya mwaka 1976 hadi 1977 na baadaye Mwendesha Mashtaka Wilaya ya Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma kati ya 1977 na 1984.

Alikuwa Mkufunzi katika Chuo cha Polisi kilichopo Kurasini Dar es Salaam, kati ya mwaka 1984 na 1987 kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi ya Magomeni na Kinondoni. Manumba baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia 1987 hadi 1993.

Kati ya mwaka 1993 na 1995, alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi kati ya 1995 na 1996.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Kukabiliana na Uhalifu wa Kughushi Makao Makuu ya Upelelezi mwaka 1996 na 1997 na baadaye kuwa Mkuu wa Kitengo cha Usalama, Intelijensia na Kupambana na Biashara ya Dawa za Kulevya kwenye Makao Makuu ya Upelelezi kuanzia 1997 hadi 2001. 

Mwaka 2001 hadi 2006 aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na kuanzia mwaka 2006 hadi anastaafu, alikuwa Mkurugenzi wa idara hiyo.

Mapema Januari 2013, jina la DCI Manumba lilitawala vyombo vya habari baada ya hali yake kuwa mbaya na kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Januari 26 mwaka huo, alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg. Alirejea nchini Aprili 23, 2013 baada ya miezi miwili na kusema ni mkono wa Mungu uliomfanya apate nafuu kubwa baada ya juhudi kubwa za madaktari kupigania uhai wake.