Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 14Article 557416

Habari Kuu of Tuesday, 14 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Teknolojia kutoa matokeo ya sensa ndani ya mwezi mmoja

Dk. Albina Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema Sensa ya Mwaka 2022 itahusisha ukusanyaji wa taarifa za watu na makazi kote nchi nzima na kwa kutumia teknolojia itakayo toa matokeo ndani ya mwezi mmoja.

Dk Chuwa amesema jijini Dodoma kwamba tofauti na sensa za awali zilizohusisha utumiaji wa teknolojia ya makaratasi kwa asilimia 95 sensa hii itakusanya taarifa za watu, umri, jinsi, uraia, makazi, shughuri za kiuchumi nchi nzima.

“Awali uchambuzi wa sensa uliishia katika ngazi ya Wilaya na kukadiria taarifa za maeneo ya ngazi ya kata kwa asilimia. Utaratibu wa Sasa tutakusanya taarifa hadi ngazi ya kitongoji tukihusisha taarifa za majengo yote mijini na vijijini,” amesema Dk Chuwa.

Kwa mujibu wa Mtakwimu Mkuu, taarifa za majengo zitahusisha idadi ya majengo, aina za paa, kuta na shughuri zote zinazofanyika katika kila jengo mijini na vijijini nchi nzima.

Dk Chuwa amesema zoezi jingine kubwa ni kuchukua anwani za makazi katika maeneo yote nchi nzima, taarifa hizo zitawekwa kwenye kanzi data.

“Ni fursa hususani kwa akina mama ukiwa na taarifa hivi ni rahisi kupata mikopo. Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika, hakuna nchi nyingine Afrika imefanya haya,” amesema Dk Chuwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Watakwimu katika Bara la Afrika na kuongeza kuwa taarifa za mipaka ya mitaa, shia na vitongoji sasa vitakuwa rasmi.