Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 28Article 560089

Habari Kuu of Tuesday, 28 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Tozo za Miamala bado moto, Askofu ampa Rais kilio cha wananchi

Askofu ampa Rais kilio tozo miamala ya simu Askofu ampa Rais kilio tozo miamala ya simu

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Elim Pentekoste Tanzania (KEPT), Peter Konki, ameiomba serikali kuendelea kuangalia tena tozo za miamala ya simu, kwani wananchi bado wanaendelea kunung’unika.

Alitoa ushauri huo mjini Babati wakati wa Jubilee ya miaka 75 ya kanisa hilo iliyofanyika Uwanja wa Kwaraa.

Askofu Konki alisema ni vizuri serikali ikawasikiliza wananchi juu ya manung'uniko waliyonayo ya tozo, kwamba wengi wao bado hawamudu gharama za makato.

"Rais Samia Suluhu Hassan namwomba awasikilize wananchi wanaumia sana juu ya tozo, siyo vizuri kuongoza watu wanaolalamika. Itafutwe namna ya kufanya," alisema Askofu Konki.

Kiongozi huyo wa kiroho alisema tozo bado zinawaumiza Watanzania, hivyo ni vizuri washauri wa Rais Samia waone namna nzuri ya kumshauri juu ya suala hilo ili afanye maamuzi ambayo yatakuwa na baraka.

Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaochukia watu kwa kuikosoa serikali na kuwa maadui.

Konki alisema mtu anapoikosoa serikali siyo vizuri kumchukia kwa kuwa anakuwa na nia nzuri ili serikali iweze kujirekebisha na kuboresha huduma.

Wakati huo huo, aliwashauri wananchi kuendelea kutumia njia ya maombi ili kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona, huku akimwagia sifa Hayati Rais John Magufuli kuwa aliacha historia ya imani na kuhamasisha Watanzania kumwomba Mungu ili kuutokomeza ugonjwa huo.

"Watanzania tuna tabia ya kujisahau, tunatakiwa kuomba ili Mungu atuepushe na corona, maombi ya kanisa ni muhimu sana," aliongeza Askofu Konki.

Aliwataka wananchi kumwombea Rais Samia ili akifanya maamuzi yawe na maslahi mapana kwa Taifa.

Kuhusu Jubilee hiyo, Askofu Konki alisema wanakumbuka jitihada za Wamisionari kutoka Uingereza na nchi nyingine za kiafrika walivyounga mkono kanisa hilo.

Alisema wamedhamiria kufufua miundombinu ya afya hasa Zahanati ya Msola iliyopo Wilaya ya Bagamoyo, ambayo ilianzishwa na Wamisionari chini ya kanisa hilo.

Alisema miundombinu sasa hivi imeimarishwa kutokana na juhudi za Wamisionari walizozifanya huko nyuma hasa barabara zilijengwa kwa kiwango mpaka sasa zinatumika.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange, alisema serikali inatambua mchango wa taasisi za dini. Aliahidi kuendelea kushirikiana na taasisi za dini na atakuwa akiwatumia kuhamasisha shughuli za maendeleo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Dk. Emmanuel Mkony, alisema asilimia 60 ya Watanzania endapo wakichanja ugonjwa huo utakuwa umedhibitiwa.