Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542209

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tril 13/- kutumika miradi ya maendeleo

SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha 2021/22, Sh bilioni 13,326 zinakadiriwa kutumika kugharamia miradi ya maendeleo zikiwa ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya Serikali.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema hayo bungeni jana wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.

Alisema kati ya kiasi hicho, Sh bilioni 6,180.0 ni matarajio ya mapato ya ndani, Sh bilioni 4.190 ni mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara na Sh bilioni 2.955 ni misaada na mikopo nafuu kutoka nje ya nchi.

Mwigulu alisema sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo itatumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kwamba, miradi mingine ya maendeleo, itaendelea kugharamiwa kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) pamoja na utaratibu wa kampuni maalumu.

Alisema serikali itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi utakaowezesha kupanuka kwa wigo wa kodi.

Alisema serikali pia itaimarisha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiyari ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na kutoa elimu kwa umma na kuendelea kurasimisha sekta isiyo rasmi.

Alisema serikali itaimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; pamoja na kuoanisha na kuboresha tozo na ada mbalimbali.

Dk Mwigulu alisema serikali pia itaendelea kutekeleza Mfumo wa Dirisha Moja la Kielektroniki (TeSWS) ili kurahisisha upitishaji wa mizigo katika vituo vya mipakani na kupunguza gharama za kufanya biashara nchini.

Alisema serikali itaendelea kusimamia Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG), kusimamia malipo ya tozo na ada ili kuhakikisha kuwa michango stahiki inawasilishwa kwa wakati kwenye mfuko mkuu wa hazina ya serikali.

Mwigulu alisema serikali itaimarisha usimamizi wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo zinazopelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo kupitia mfumo wa uratibu wa fedha zinazopelekwa moja kwa moja kwa watekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha maandalizi ya miradi ya maendeleo.

“Mpango huu ni wa kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya "Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu"alisema.

Alisema utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2021/22 unalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuimarisha utulivu wa viashiria vya uchumi jumla na kasi ya ukuaji wa uchumi.

Join our Newsletter