Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540679

xxxxxxxxxxx of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tume kuanzisha kituo cha wataalamu Tehama

TUME ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inakusudia kuanzisha kituo cha kitaifa cha maendeleo ya wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kitakachojengwa jijini Dodoma.

Kuanzishwa kwa kituo hicho kunalenga kupanua upeo wa wataalamu na kuwawezesha kufuatilia na kumudu kasi ya mabadiliko katika nyanja ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Samson Mwela, alibainisha hayo kwa waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam jana.

Alisema tume hiyo inakusudia kuanzisha vituo vya teknolojia kwa ajili ya vijana na wafanyabiashara ndogo katika kanda tano za Kati, Kaskazini, Kusini, Pwani na Magharibi.

Ofisi za kanda zitakuwa Dar es Salaam, Pwani (Kanda ya Pwani), Dodoma (Kati), Arusha (Kaskazini), Mwanza (Magharibi) na Mbeya (Kusini).

“Mpango wa kufikisha huduma kwenye kanda hizo umelenga kupunguza msongamano wa utoaji huduma makao makuu ya tume,” alisema.

Akaongeza: “Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kuifanya nchi yetu kuwa mahala pa kuvutia zaidi uwekezaji na ubunifu wa kidigitali,”

Alisema katika kila kanda wananatarajia kuanzisha kituo cha ubunifu na vituo hivyo, vitasaidiana na kituo cha kitaifa cha Dodoma.

Alisema vituo hivyo vitaiwezesha tume kuwafikia wananchi wengi, kuweka msingi wa ukuaji wa uchumi wa kidigiti na kuifanya Tehama kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Mwela, mpango unatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, taasisi za mafunzo ya ufundi, Tume ya Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wadau wa sekta binafsi.

Alisema tume na wizara wanakusudia kuanzisha maabara ya matengenezo kwa ajili ya kukarabati vifaa chakavu vya Tehama na kuhuisha baadhi ya programu tumizi ili ziweze kutumika tena.

“Tume inafanya yote hayo lengo likiwa ni kupata mifumo yetu ya Tehama inayolingana na mazingira ya Kitanzania kuliko mifumo mingi ambayo tumekuwa tukichukua nje ya nchi kwa gharama kubwa,” alisema.

Join our Newsletter