Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 26Article 539869

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

UMMY AKIRI HALI TETE AJIRA ZA WALIMU

UMMY AKIRI HALI TETE AJIRA ZA WALIMU UMMY AKIRI HALI TETE AJIRA ZA WALIMU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu amesema pamoja na wizara kutumia kigezo cha kujitolea kupata ajira za walimu, bado kuna changamoto ya baadhi yao kughushi barua.

Pia amekiri ajira za walimu hali ni tete, lakini aliahidi kutenda haki katika kutoa ajira hizo.

Ummy alikuwa akitoa majibu ya nyongeza kutokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Longido, Dk Steven Kiruswa (CCM) aliyeomba serikali iangalie namna ya kuwaajiri walimu wanaojitolea.

“Ni kweli kigezo kikubwa tunachokitumia na walimu wa kujitolea, lakini nikiri kuwa na hao wa kujitolea tumeshapokea malalamiko kuwa kuna wengine wameleta barua feki za kusema wanaojitolea wakati hawajitolei.

“Pia tumepokea maelekezo yako (Spika Job Ndugai). Hali ni tete, nafasi ni 6,946, mpaka juzi (Jumapili) waliokuwa wameomba ni 89,958 suala hili naomba utuamini serikali tutatenda haki, hata hao wanaosema wanajitolea tutawachambua kama ni kweli wanaojitolea,” alisema Ummy.

Aliongeza, “Lakini pia kuna walimu wamemaliza mwaka 2012, 2013, 2014 na 2015 hajawaajiriwa, upo pia mtazamo ndani ya wizara tuwaangalie hawa nao ambao wamemaliza siku nyingi wanajitolea na hawajapata ajira kwa sababu muda wao wa kuajiriwa serikalini unapungua maana lazima waajiriwe kabla ya miaka 45.

“Mheshimiwa Spika naomba uiamini serikali, hali ni tete walioomba na wenye vigezo ni wengi nafasi ni chache, Lakini tutatenda haki kama ulivyoelekeza bila kubagua dini, kabila jinsia wala upendeleo wala nafasi ya mtu yeyote.”

Spika Job Ndugai amesema Bunge litafuatilia kwa karibu ajira zinazotolewa na serikali ili zitolewe kwa uwazi huku zikibeba sura ya kitaifa.

Awali, Naibu Waziri, David Silinde akijibu swali la nyongeza la Dk Kiruswa alisema serikali ingetamani walimu wote wanaojitolea waajiriwe, lakini haitaweza kutokana na uhaba wa nafasi za ajira.

“Kwa mfano sasa hivi tuliomba taarifa za walimu wote wanaojitolea mashuleni tukaletewa orodha ya walimu 70,000 wanaojitolea wakati nafasi zikizotangazwa na serikali ni 6,000 mnaweza kuona ukubwa wa changamoto,” alisema.

Alisema Mei 2021, Ofisi ya Rais-Tamisemi ilitangaza ajira 6,949 za walimu wa shule za msingi na sekondari ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu.

Join our Newsletter