Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 23Article 559168

Habari Kuu of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

UN yaisifu Tanzania kudumisha amani, kuhifadhi wakimbizi

UN yaisifu Tanzania kudumisha amani, kuhifadhi wakimbizi UN yaisifu Tanzania kudumisha amani, kuhifadhi wakimbizi

MWAKILISHI wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Jacquelin Mahon amesema Tanzania inastahili sifa kwa kudumisha amani, kuzisaidia nchi kupata uhuru na kuhifashi wakimbizi.

Mahon alisema hayo wakati wa Kongamano la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani lililofayika katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dar es Salaam.

Aliipongeza Tanzania kwa namna inavyodumisha amani yake na akaisifu kwa namna ilivyojitolea kwenye uhuru katika eneo la Kusini mwa Bara la Afrika sanjari na kuhifadhi wakimbizi 300,000 waliozikimbia nchini zao kutokana na ukosefu wa amani.

Alisema mchango wa Tanzania unapaswa kutambuliwa, kuheshimika na mataifa mbalimbali yaliyopo katika bara hilo kutokana na viongozi wake kujitoa na wakati mwingine kusaidia kupatikana kwa amani katika mataifa hayo.

Aidha, alisema kaulimbiu ya Siku ya Amani Kimataifa mwaka huu inayosema, ‘Kupona vizuri kwa ajili ya Dunia ya usawa wa haki na iliyo endelevu,’ inapaswa kuwakumbusha watu wote kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa Covid-19 huku wakiwasaidia wagonjwa wa ugonjwa huo ili wapone vizuri.

“Leo tunamtambua na kumshukuru hayati Koffi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa mtetezi wa haki za binadamu, haki na sheria, ni mambo mengi na mazuri aliyafanya wakati wa uhai wake hivyo ili kumuenzi tunapaswa kumkumbuka kwa vitendo kwa kuilinda haki ya kila mtu,” alisema Mahon.

Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda alisema Siku ya Amani ya Duniani ilianza mwaka 1981 ikitimiza miaka 40 hadi sasa.

Profesa Bisanda alisema OUT waliitumia kwa kujadili masuala muhimu matatu ambayo ni elimu, afya na uchumi aliyoyasema kuwa ni chachu ya amani kwa kila mwanadamu.

Alisema wakati dunia ikiendelea kupambana na janga la Covid- 19 Watanzania wanapaswa kujitokeza kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo ili kujilinda.

Profesa Bisanda alisema Tanzania ilipokea dozi za chanjo hiyo, lakini idadi ndogo ya wananchi ikijitokeza kuchanja, suala alilosema ni sawa na kujinyima amani ya mioyo na kujiweka katika hatari ya kupata maambikizi, tofauti na mataifa mengine ambayo yameipokea chanjo hiyo kwa upekee.

Katika kongamano hilo, watu mbalimbali walitunukiwa vyeti kutokana na mchango wao katika kudumisha amani akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Peter pamoja na mwanasiasa mkongwe Paul Kimiti.