Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 25Article 553513

Siasa of Wednesday, 25 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

UVCCM yampongeza Samia fursa za biashara nje 

UVCCM yampongeza Samia fursa za biashara nje  UVCCM yampongeza Samia fursa za biashara nje 

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umempongeza Rais Samia Suhuhu Hassan kwa kuimarisha na kufungua fursa za kibiashara na nchi jirani kwa kuendeleza utaratibu wa viongozi watangulizi wake.

Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenani Kihongosi alisema ziara za Rais Samia katika mataifa jirani zinadumisha na kuendeleza ushirikiano na nchi jirani hizo kama walivyofanya watangulizi wake katika awamu ya kwanza hadi ya tano.

“Ziara za Rais Samia katika nchi mbalimbali zikiwemo za kikanda ni kuimarisha ushirikiano na nchi jirani kama walivyofanya watangulizi wake,” alisema Kihongosi.

Katibu huyo alisema mfumo wa kudumisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa ulifanyika tangu wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alifanya ziara Ghana kuonana na Nkwame Nkrumah na Afrika Kusini kwa Nelson Mandela na hata alienda mara kadhaa Ulaya.

“Hata Mzee Ali Hassan Mwinyi na hayati Benjamin Mkapa walisafiri katika nchi mbalimbali za kikanda, Afrika, Ulaya na maeneo mbalimbali katika kudumisha ushirikiano kwa Tanzania si kisiwa, inahitaji nchi hizo kama ambayo zinaihitaji Tanzania katika kujenga uchumi na kuleta maendeleo,” alieleza.

Kihongosi alisema utaratibu huo wa taasisi ya Rais, umeendelezwa pia na Jakaya Kikwete hata hayati John Magufuli ambaye alitembelea Afrika Kusini, Zimbabwe, Rwanda na nchi nyingine za ukanda huo.

Alitoa mfano wa ziara ya Rais Samia nchini Kenya ilivyosaidia kurudisha uhusiano mzuri wa kibiashara baina ya nchi mbili hizo ambao ulizorota kwa muda kidogo.

Alieleza kuwa kitendo cha kwenda kuhudhuria sherehe za kumwapisha Rais Hakainde Hichilema pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM jana nchini Zambia, ni cha kudumisha uhusiano kutokana na ukweli kwamba nchi hiyo na nyingine za ukanda huo zimewahi kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake, hayati Magufuli, Kikwete, Mkapa na wengine.

Aliwataka vijana wa chama hicho kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuwa wazalendo kufanya kazi kwa bidii, lakini pia kufuata maelekezo ya madaktari katika kujikinga na Covid-19 na kuchanja ili kulinda familia zao.

Aliwataka vijana kusimama imara, kulinda heshima ya chama, serikali na viongozi wake kuanzia Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na watendaji wengine serikalini huku wakisimamia misingi ya uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.