Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 22Article 573388

Habari Kuu of Monday, 22 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Uamuzi mapingamizi kesi ya kina Mbowe leo

Freeman Aikael Mbowe, Mwenyeketi wa CHADEMA Freeman Aikael Mbowe, Mwenyeketi wa CHADEMA

Mahakama Kuu Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo inatarajiwa kutoa uamuzi utakaomaliza mvutano wa mawakili kuhusiana na upokewaji wa kielelezo cha upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Mbowe na wenzake hao, Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya wanakabiliwa na kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga.

Uamuzi huo unahusu pingamizi la mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, ambao walipinga kupokewa kwa kitabu cha kumbukumbu za mahabusu (Detantion Register – DR), cha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, cha mwaka 2020, kiwe kielelezo cha ushahidi upande wa mashtaka.

Upande wa mashtaka unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando uliiomba mahakama hiyo ikipokee kitabu hicho kuwa kielelezo cha ushahidi wake, kupitia kwa shahidi wa pili katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, Ditektivu Koplo Ricardo Msemwa.

Hata hivyo jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Peter Kibatala lilipinga kitabu hicho kupokewa, huku wakitoa hoja tatu za pingamizi lao

Walidai kwamba hakuna amri ya mahakama ya kukiondoa mahakamani kielelezo hicho kwa kuwa kilishapokewa mahakamani katika kesi ndogo iliyohusu uhalali wa maelezo ya mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa.

Pia walidai kuwa kielelezo hicho tayari kilishatolewa uamuzi katika kesi hiyo ndogo na kwamba ilikikataa na hivyo mahakama haiwezi kukizungumzia tena na hoja ya tatu walidai kuwa kwa kuwa mahakama ilishakitolea uamuzi, basi upande wa mashtaka hauna mamlaka ya kukileta tena mahakamani.

Kesi hiyo iko katika hatua ya usikilizwaji wa kesi ndogo, ndani ya kesi ya msingi iliyoibuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga mahakama hiyo isipokee maelezo yanayodaiwa kutolewa na mshtakiwa Ling’wenya, wakati akihojiwa na askari Polisi, Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine jopo la mawakili wa utetezi walipinga kupokewa maelezo hayo kwa madai kuwa mshtakiwa huyo hakutoa maelezo kituoni hapo, kwa kuwa hajawahi kufikishwa kituoni hapo na kwamba hakuwahi kutoa maelezo yake popote.