Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 27Article 554011

Habari Kuu of Friday, 27 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Uamuzi tozo miamala ya simu Agosti 31

Uamuzi tozo miamala ya simu Agosti 31 Uamuzi tozo miamala ya simu Agosti 31

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kuwa serikali bado inalifanyia kazi suala la tozo kupitia miamala ya simu na kwamba uamuzi utatangazwa Agosti 31, mwaka huu.

Alisema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara baada ya kukagua ujenzi wa jengo katika Bandari ya Karema katika mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Tanganyika, mkoa wa Katavi ambako alianza ziara ya siku tatu mkoani humo.

Tozo hizo zinatarajiwa kuiingizia serikali Sh trilioni 1.254 ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti ya Sh trilioni 36.68 katika mwaka huu wa fedha.

Majaliwa jana alisema serikali itafanya uamuzi kuhusu hizo tozo na kwamba kuanzishwa kwake hakukuathiri shughuli za kifedha katika miamala ya simu kwa kuwa takwimu zinaonesha kiwango kiliendelea kuwa kama cha zamani.

Alisema tangu tozo hizo zilipoanzishwa katikati ya mwezi uliopita, serikali imeshapata zaidi ya Sh bilioni 48.4 na kwamba Sh bilioni 37 kati ya hizo zimetengwa zijenge madarasa 560 na vituo vya afya 150 nchini nzima.

Alisema Sh bilioni 22.5 tayari zimepelekwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili zitumike kutekeleza miradi.

Wakati huohuo, Majaliwa jana alizindua kiwanda cha kuchambua pamba cha kampuni ya NGS Investment Ltd na akawataka wakulima watumie fursa hiyo kuongeza mashamba kwa kuwa kuna uhakika wa soko.

Alizindua kiwanda hicho katika kijiji cha Ifukutwa, wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi.

Majaliwa alisema zao la pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, hivyo serikali itaendelea kulisimamia katika hatua zote.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuinua uchumi wa nchi kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu ili itumike na wananchi kusafirisha mazao na kusambaza bidhaa.