Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 559003

Dini of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

‘Uaskofu si kazi ya siasa’

‘Uaskofu si kazi ya siasa’ ‘Uaskofu si kazi ya siasa’

ASKOFU Henry Mchamungu amesema uaskofu si kazi ya siasa bali ya utumishi na kuwaomba waumini wamuombee yeye na mwenzake waliowekwa wakfu na kusimikwa jana kuwa maaskofu wasaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ili wapate nguvu na kutiwa moyo wa kufanya kazi ya Bwana.

Mchamungu alisema hayo jana baada ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Ruwa’ichi kuwasimika na kuwaweka wakfu jana katika Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Msimbazi.

Aliwaomba maaskofu wengine wote kwamba kutokana na uzoefu na mang’amuzi yao katika utume huo na kama wachungaji wa kanisa, wawasaidie kufanya kazi zao vizuri kama wachungaji wa kanisa.

“Nanyi wengine, watawa pamoja na walei, tunaomba ushirikiano wenu ili kazi hii ambayo Mwenyezi Mungu ametukabidhi tuweze kuitekeleza vizuri.

Naombeni sala zenu ili niwe mwaminifu kwa kanisa, kwa Baba Mtakatifu na kutunza umoja wa kanisa,” alisema Askofu Mchamungu.

Kwa upande wake, Askofu Ruwa’ichi alisema uaskofu ni utume na si heshima na cheo, hivyo maaskofu hao wameingia kwenye kazi ya utume moja kwa moja.

“Napenda kuungana nanyi kumshukuru Mungu kwa siku hii nzuri ambayo tumepata Maaskofu Wasaidizi wawili wapya. Wanaanza kazi wakibeba hadhi ya kuwa Mavika Jenerali, kwa hiyo wanawajibika kama Manaibu wa Askofu kwa jimbo lote,”alisema Askofu Ruwa’ichi.

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga, aliwapongeza maaskofu hao wapya na kuwakabidhi vitendea kazi vya Baraza la Maaskofu.