Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540283

Habari Kuu of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa

Ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa Ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa

MAKALA haya yanaangalia ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataiafa na yamegawanyika katika sehemu tano ambazo ni Utangulizi, Shughuli za Ubidhaishaji wa Kiswahili, Wajibu wa Serikali, Wajibu wa Mtu Binafsi na Hitimisho.

Katika makala haya kuna baadhi ya istilahi zinazohitaji ufafanuzi. Istilahi hizo ni ubidhaishaji, taifa na mataifa. Ubidhaishaji ni kufanya kitu kiwe bidhaa na kiweze kuuzwa na kutoa faida kwa mwenye kitu hicho. Bidhaa kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ni vitu aghalabu vya thamani vinavyouzwa na kununuliwa katika biashara.

Taifa kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ni jamii ya watu wanaoishi katika nchi moja na wanaounganika kutokana na matukio ya kihistoria; mfumo wa uchumi na utamaduni chini ya serikali moja. Hivyo, kubidhaisha Kiswahili kitaifa maana yake ni kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa ndani ya taifa linalohusika na kwa muktadha huu ni ndani ya nchi yetu ya Tanzania.

Dhana ya mataifa inahusisha nchi nyingine zaidi ya nchi mnamoishi. Kubidhaisha Kiswahili kimataifa ni kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa nje ya taifa letu la Tanzania, yaani, katika nchi za Afrika Mashariki, Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC, Afrika na dunia nzima kwa ujumla.

Katika makala haya tutajadili namna Kiswahili kinavyokuwa bidhaa kwa kuangalia fursa zilizopo hapa nchini na nje ya nchi. Tutaelezea wajibu wa serikali katika kubidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa na kuonesha wajibu wa mtu binafsi katika kuzipata fursa hizo.

Lengo kama nchi ni kutaka tukiuze Kiswahili ili kitunufaishe kama taifa na na hata watu binafsi. Kiswahili kinazidi kukua na kuenea duniani kote. Aidha, Kiswahili kinazidi kupendwa na kupewa fursa na watu na mataifa mbalimbali. Kwa hiyo, Kiswahili sasa ni bidhaa inayojiuza na siyo inayojitembeza, hivyo basi tuendelee kukiuza ili kitufae.

Shughuli za Ubidhaishaji wa Kiswahili

Mchakato wa ubidhaishaji wa Kiswahili unahusisha shughuli mbalimbali ambazo Watanzania wenye utaalamu wa lugha ya Kiswahili wanaweza kuzifanya. Shughuli hizo ni kama vile ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, uandishi wa vitabu, tafsiri na ukalimani, uandishi na utangazaji wa habari, shughuli za sanaa n.k.

Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni

Kufundisha Kiswahili kwa wageni ndani ya nchi na nje ya nchi ni moja ya shughuli za ubidhaishaji wa Kiswahili. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni – Hatua ya Awali, Kati na Juu, kuna mikabala mingi ya ufundishaji na ujifunzaji wa lugha.

Hata hivyo, mkabala unaotumika sasa ni ule wa ufundishaji na ujifunzaji wa lugha unaozingatia mchakato wa kimawasiliano na utamaduni unaoambatana na lugha inayofundishwa. Huu unaitwa mkabala wa kimawasiliano. Mkabala huu unaweka mkazo katika umahiri wa kimawasiliano kwa mjifunzaji, na unasisitiza umuhimu wa kuvielewa vipengele vya kiisimu, kiisimujamii, kimuktadha na mbinu zinazotumika kufundishia na kujifunzia.

Watanzania wenye taaluma hii wanaweza kuutumia mkabala huu kwa kuwafundisha wageni wa ndani na nje ya nchi. Mahitaji yao si kuwa wabobezi wa lugha ya Kiswahili bali ni kujua Kiswahili kwa ajili ya mawasiliano. Nchini Tanzania, kila mwaka tunapokea wageni mbalimbali wanaokuja kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile uwekezaji, utalii, shughuli za hisani, kufanya miradi, mikutano, mafunzo na kufanya kazi.

Wengi wa wageni hawa, huhitaji kujifunza Kiswahili ili watakapokuwa katika shughuli zao waweze kuwasiliana na wenyeji wao. Kwa maana hii, walimu wa kufundisha Kiswahili kwa wageni wanahitaji kuchangamkia fursa hii ya kuwafundisha wageni hawa.

Nje ya taasisi kubwa zinazofundisha Kiswahili kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), wataalamu wengine wenye ujuzi huu wanatakiwa kujipanga kwa kuwatafuta wageni kwa njia za mbalimbali kama vile mitandao, matangazo na kufungua vituo vya kufundishia wageni.

Aidha, walimu watatakiwa kujua njia mbalimbali za ufundishaji wa wanafunzi. Mfano, katika kipindi hiki cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19) walimu wanatakiwa kujua namna ya kutumia mitandao ili waweze kulipata soko kwa kufundisha kwa njia hii. Kwa kufanya hivyo, walimu watakuwa wametumia vyema fursa ya kukiuza Kiswahili kama bidhaa na Kiswahili kitawanufaisha na kulinufaisha taifa kwa ujumla.

Uandishi wa Vitabu

Katika ubidhaishaji wa Kiswahili kitaifa na kimataifa lipo pia suala la uandishi wa vitabu. Uandishi wa vitabu uko wa aina mbalimbali, mfano, vitabu vinavyoweza kutumiwa katika mitaala ya masomo ya Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu, vitabu vya kufundisha Kiswahili kwa wageni, vitabu vya kujiburudisha kama vile vya hadithi fupi, riwaya, tamthiliya, tenzi, mashairi, hadithi za watoto n.k.

Kwa maana hii, waandishi wa vitabu wanatakiwa kuandika vitabu kwa ajili ya kuwauzia wanafunzi, taasisi na wasomaji wengine wa vitabu ndani na nje ya nchi. Aidha, waandishi wanaweza kuandika vitabu vya nyanja mbalimbali kwa Kiswahili. Nyanja hizo ni kama vile za sheria, tiba, biashara na uchumi, sanaa, michezo, historia, sayansi na teknolojia, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) n.k. Kwa kufanya hivi Kiswahili kitakuwa kimetumika kama bidhaa kitaifa na kimataifa na kuwanufaisha waandishi hao na taifa kwa ujumla kutokana maduhuli ya serikali.

Tafsiri na Ukalimani

Kiswahili kimekuwa lugha ya kimataifa kwani kinatumika katika shughuli na mikutano mbalimbali ya kimataifa kama vile katika Umoja wa Afrika (AU), Bunge la Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC, nchi zinazochimba madini ya almasi na taasisi nyingine kubwa za kimataifa.

Kutokana na hatua hii, wakalimani na wafasiri wanahitajika ili waweze kuhudumia katika shughuli na mikutano ya taasisi hizi pale inapojitokeza. Hii nayo ni fursa kwa Watanzania wenye weledi na taaluma hizi kushiriki katika shughuli hizi. Jambo muhimu ili uweze kunufaika na fursa hii ni kukijua Kiswahili vizuri pamoja na lugha nyingine za kimataifa kama vile Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kireno, Kichina, Kijerumani n.k.

Aidha, ili aweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi, mtaalamu huyo anapaswa kujua istilahi mbalimbali kama vile za siasa, uchumi, utamaduni, sayansi na teknolojia, TEHAMA n.k.

Uandishi na Utangazaji wa Habari

Fursa nyingine inayotokana na kukibidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa ni uandishi na utangazaji wa habari. Mpaka sasa twakwimu zinaonesha kuwa kuna idhaa takribani 39 nje ya Afrika Mashariki zinazotangaza kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Kutokana na kasi ya kukua kwa lugha ya Kiswahili, idadi hiyo inaweza kuongezeka maradufu. Nchi nyingi zaidi duniani zinatamani kufungua idhaa mbalimbali zitakazorusha matangazo yao kwa lugha ya Kiswahili. Kutokana na hali hii, kuna uwezekano mkubwa kwa wanahabari kutoka Tanzania kupata fursa hizi.

Hii ni fursa nyingine muhimu kwa waandishi na watangazaji wa habari. Wanataaluma wa tasnia ya habari wanatakiwa kuchangamkia fursa hii. Kwa vyovyote vile, watangazaji wazuri watakaohitajika ni wale wanaofahamu vizuri lugha ya Kiswahili, na bila shaka, wanaotoka Afrika Mashariki, na hasa kutoka Tanzania.

Hivyo, watangazaji na waandishi wa habari, watoa taarifa na wahariri wa habari watanufaika na fursa ya kukitumia Kiswahili kama bidhaa. Ikumbukwe kuwa fursa hizi zitakuwa ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, wanahabari wasilale bali wachangamkie fursa hizi pindi zinapojitokeza.

Aidha, wanahabari wa Tanzania wanaweza wakaandaa vipindi mbalimbali, vya kuelimisha na kuburudisha umma wa watazamaji au wasikilizaji na kuviuza katika idhaa mbalimbali duniani wakafaidika na maslahi yanayotokana na shughuli hiyo.

Itaeendelea wiki ijayo.

Join our Newsletter