Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542161

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Uhamiaji yanasa Wahabeshi 46

IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Pwani inawashikilia raia wa Ethiopia 46 kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ya uhamiaji walikohifadhiwa raia hao, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Pwani, Omary Hassan alisema raia hao wote wanaume wana umri kati ya miaka 18 na 30.

Hassan alisema tukio hilo lilitokea Juni 9 majira ya saa 8:00 mchana eneo la Razaba kata ya Makurunge wilaya ya Bagamoyo ambapo walikutwa wakisubiri usafiri.

"Taarifa za kiintilejensia zinaonesha kuwa wahamiaji hao haramu waliingia nchini kwa kutumia usafiri wa boti wakitokea nchi jirani na walikuwa wana lengo la kwenda Afrika Kusini,"alisema Hassan.

Aidha alisema baadaye walitembea kwa miguu umbali mrefu mpaka sehemu waliyokamatwa ambapo walikuwa peke yao na hawakuwa na mwenyeji ambaye ni Mtanzania.

"Bado tunaendelea kuwatafuta Watanzania ambao walihusika na tukio hili kwani haiwezekani waje wenyewe bila ya kuwa na mwenyeji," alisema.

Aliwataka wananchi wa mkoa wa Pwani kuendelea kutoa taarifa juu ya uwepo wa wahamiaji haramu wanaosafirishwa au waliohifadhiwa na taarifa watakazotoa hizo zitakuwa za usiri mkubwa na hatua zitachukuliwa haraka.

Alibainisha kuwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kifungo cha miaka 20 jela au faini ya Sh milioni 20 ama adhabu zote mbili kwa pamoja na watafilisiwa mali zitakazotumika ikiwa ni pamoja na nyumba na vyombo vya usafiri vitakavyotumika. Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Join our Newsletter