Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 13Article 585451

Diasporian News of Thursday, 13 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Ujenzi barabara za kilometa 220 kuifungua Pemba

Ujenzi barabara za kilometa 220 kuifungua Pemba Ujenzi barabara za kilometa 220 kuifungua Pemba

Serikali ya Zanzibar imesema inakusudia kuifungua Pemba kiuchumi na uwekezaji kwa kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 220 ikiwamo ya Chakechake hadi Wete ambayo imekwama kwa muda mrefu.

;Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka 58 ya mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya mawasiliano na usafirishaji.

Alisema mikakati ya kuifungua Pemba kiuchumi na uwekezaji ni sehemu ya malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane, ambapo kutakuwa na ujenzi wa miundombinu Unguja na Pemba.

Alisema barabara zenye urefu wa kilometa 4959.9 zinatarajiwa kujengwa katika kipindi cha miaka mitatu ikiwamo Barabara ya Chakechake hadi Wete yenye urefu wa kilometa 220. Kassim alisema ujenzi wa barabara hiyo kwa kiasi kikubwa utafanikisha malengo ya Serikali ya Zanzibar Awamu ya Nane katika uwekezaji wa maeneo huru ya uchumi Micheweni, Pemba.

“Miongoni mwa mambo ambayo yamechelewesha kuifungua Pemba kiuchumi na uwekezaji ni ukosefu wa miundombinu ya barabara za kuyafikia maeneo huru ya uchumi yaliyopo Micheweni Pemba.” ‘’Serikali ya Zanzibar tumejipanga kuimarisha miundombinu ya barabara zinazokwenda vijijini pamoja na barabara kuu zitakazounganisha mikoa yote, ambapo kwa upande wa Pemba tumeweka kipaumbele cha kwanza kufanikisha azma hiyo,’’ alisema.

Aidha, Rahma alisema upembuzi yakinifu kuhusu mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Pemba umekamilika na kwa sasa wizara hiyo ipo katika mchakato wa kutafuta wakandarasi wa mradi huo.

Alisema kufanikisha ujenzi wa kiwanja hicho cha ndege pamoja na ujenzi wa Bandari ya Mkoani, Chakechake na Wete ni mikakati ya kuifungua Pemba kiuchumi na uwekezaji. ‘’Serikali ya Zanzibar Awamu ya Nane imejipanga kufikisha maendeleo katika Kisiwa cha Pemba katika sekta mbalimbali ikiwamo uwekezaji na miundombinu ya usafirishaji na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Pemba chenye hadhi ya kimataifa,’’ alisema.a