Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558466

Habari za Mikoani of Monday, 20 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ukatili wa kijinsia kwa wanawake tishio Kilimanjaro

Ukatili wa kijinsia kwa wanawake tishio Kilimanjaro Ukatili wa kijinsia kwa wanawake tishio Kilimanjaro

ASILIMIA 40 ya wanawake wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 40 wamebainika kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani Kilimanjaro, jambo linalosababisha baadhi yao kuishi kwa hofu katika jamii.

Hayo yalisemwa na Ofisa Mradi wa Mwanamke Imara kutoka shirika lisilo la kiserikali la Tanlap, Jackline Mollel wakati akitoa elimu ya jinsia kwa wananchi wa tarafa ya Masharti, wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Alisema zaidi ya asilimia 40 ya wanawake na wasichana kuanzia umri huo wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwamo kubakwa na kunyanyaswa kingono hali ambayo imekuwa ikiwaathiri kisaikolojia na kuishi kwa hofu.

"Changamoto kubwa inayoikabili jamii yetu ya mkoa wa Kilimanjaro hususani wilaya hii ni wimbi la vitendo vya ukatili, takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 40 ya wanawake na wasichana kati ya umri wa 15 hadi 40 wamefanyiwa ukatili, suala hili linawasababisha kushindwa kujiamini na kuishi kwa hofu," alisema.

Molell alisema wilaya ya Rombo ni kati ya wilaya zinazokabiliwa na changamoto ya matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwamo wanawake kupewa vipigo na wasichana kupewa mimba katika umri mdogo na kukatisha masomo yao.

Ofisa Tarafa ya Mashati, Hassan Ndulu alikiri kuwapo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia katika tarafa hiyo ikiwamo vipigo, wanawake kunyimwa haki ya kusimamia miradhi pamoja na migogoro ya ardhi.

Nao baadhi ya wasaidizi wa kisheria wilayani humo walisema kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia Rombo, kunatokana na uelewa mdogo wa kutoa taarifa juu ya matukio hayo katika ngazi zinazohusika ikiwamo ustawi wa jamii ili kuyashughulikia.

"Changamoto iliyopo Rombo ya ukatili wa kijinsia inachangiwa na vitu vingi ikiwamo wananchi kushindwa kutoa taarifa ya matukio hayo na ulevi uliopindukia kwa wanaume jambo ambalo limesabahisha kuwapiga na kuwabaka wanawake," alisema Mwanaidi Mkumbwa ambaye ni Msaidizi wa Kisheria Rombo.