Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 25Article 544222

Habari Kuu of Friday, 25 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ukikwepa kodi, ukinaswa kulipa maradufu

Ukikwepa kodi, ukinaswa kulipa maradufu Ukikwepa kodi, ukinaswa kulipa maradufu

SERIKALI imekubali hoja za wabunge waliopendekeza kutoza adhabu ya asilimia 100 ya kiwango cha kodi anachokwepa muhusika kupitia biashara katika bidhaa au huduma.

Akijibu hoja wakati wa kuhitimisha majadiliano ya Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema baada ya kusikia hoja za wabunge serikali imeamua kuchukua ushauri kwa kuweka kifungu kipya cha kubana ukwepaji kodi.

“Makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha leo asubuhi (jana) kati ya serikali na kamati ya bunge ni kufanya mabadiliko kwenye tuliokuwa tumependekeza kuweka asilimia 75 wamependekeza kuwa asilimia 100 ya kodi iliyotakiwa kutozwa”alisema Dk Mwigulu na kuongeza; “Kwa maana hiyo kodi itakuwa imezidishwa mara mbili ya iliyotakiwa kutozwa kama mtu huyo atakuwa amekwepa, kwa hiyo sisi kama serikali tunapokea maoni ya wa waheshimiwa wabunge na kamati ambayo ni mwakilishi wa Bunge.”

Awali akichangia muswada wa sheria hiyo, Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa (CCM) aliishauri serikali iondoe mpango wa kuondoa adhabu ya asilimia 100 kwa watakaokutwa na kosa la kuhamisha fedha (transfer price) kwa madai kuwa itasababisha hasara kwa taifa.

Silaa alisema kifungu hicho kitasababisha wanaokwepa kodi wawe huru kutorosha fedha hususani kampuni kubwa na hivyo serikali kupoteza mapato.

”Mapendekezo ya CAG serikali kusaidia TRA kuongeza nguvu kwenye suala la kusimamia kitengo cha International Unit ili kuondoa changamoto ya kupoteza fedha kupitia transfer price”alisema na kuongeza; ”Aliyeandika kifungu hili Mungu anamuona, ameandika akijua wazi haendi kukuza uwekezaji, bali kutengeneza hasara kubwa kwa taifa ambayo tulishaondokana nayo.”

Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini (CCM) alisema suala la gharama za kuhamisha fedha limeibua hisia kidogo na kuwa anadhani kama hatua za awali zilikuwa zinafanyika za kufilisi kabisa biashara, halikuwa na tija sana.

“Sasa hii inayopendekezwa si kutoadhibu, badala yake ni kurekebisha adhabu ile ya asilimia fulani. Kwa hiyo mimi kwa mawazo yangu na ningeomba Wabunge hili tuliunge mkono, kwamba maadamu hatuendi kumsamehe, lakini anakwenda kupewa adhabu isiyohusisha kufilisi kabisa, mimi nadhani ni mwelekeo mzuri zaidi, kuliko kuzungumzia kwamba huendi kufilisi halafu unafunga biashara.

“Hata wale watu waliokuwa wanalipwa kutokana na biashara ile hawatalipa bei ile, wala mapato hutayapata. Ambacho ningeomba serikali ifanye ni kujenga uwezo wa wataalamu wetu kubaini michezo ya transifer pricing; kwa sababu ninavyojua hatuna watu wenye weledi huo.

“Kwa hiyo serikali ingejizatiti kujenga uwezo wa watu wetu kwenye sekta za TRA na sekta nyingine za fedha ili kubaini vitu hivi kwa mapema zaidi.”

Wakati Sagini anachangia, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu, alisimama akiomba kumpa taarifa mzungumzaji, akisema dawa dawa pekee ya transfer pricing ni kwa serikali kusimamia vizuri sheria ya kulinda vitu vya ndani.