Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 16Article 547210

Habari za Mikoani of Friday, 16 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ukweli mchungu kuhusu mwonekano wa Dar

Ukweli mchungu kuhusu  mwonekano wa Dar Ukweli mchungu kuhusu mwonekano wa Dar

ULISHAWAHI kuingia kwa ndege mchana katika jiji mashuhuri au mji mkuu wa nchi ambayo ni mara yako ya kwanza kufika? Bila shaka uliangalia hali ya uwanja wa ndege baada ya kutua na kisha ulikuwa na hamu ya kuona mji huo mpya kwako mara tu baada ya kupanda gari la kukupeleka ulikotarajia kufikia.

Sehemu kubwa ya macho yako yalikuwa nje, kuona majengo na hali ya barabara yaani mandhari ya mji husika kwa ujumla. Mpaka unafika ulikotarajia kufika, ulishajua angalau kidogo kuhusu uzuri au ubaya wa mandhari ya mji husika.

Sasa hebu pata picha mgeni anayetua na ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam mchana, na kisha kuanza safari ya kuelekea katikati ya jiji, akapita Kiwalani, Vingunguti, maeneo ya Tazara hadi anakokwenda atakaribishwa na mandhari gani?

Sehemu kubwa ya vitu atakavyoona pembeni mwa barabara ya Nyerere ni vibanda vya mabati, makuti au magunia yanayoning’inia ambavyo pia havikupangwa vizuri.

Hali hii ndiyo pia inamgusa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na kulazimika kusema kwamba jiji hilo mashuhuri ni chafu na hivyo kuna umuhimu wa kulipanga upya.

Katika ziara yake ya kutembelea mkoa wa Dar es Makalla anasema bila kuuma maneno kwamba hajaridhishwa hata kidogo na hali ya usafi wa mkoa wake huo.

Anasema Dar es Salaam ni lango kuu la wasafiri, uso wa nchi, mkoa mkubwa wenye bandari pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa.

Anasema kuna siku alikwenda kumpokea Rais wa Botswana katika uwanja huo wa Julius Nyerere na kwamba kuanzia eneo hilo la uwanja wa ndege mpaka Mnazi Mmoja, yeye na mgeni wake walichokuwa wanashuhudia ni takataka za moshi wa kuni na mkaa na vibanda vilivyokaa bila mpangilio na hivyo kuonekana ni uchafu.

“Ni aibu. Kosa si la wale wanaofanya ile biashara ila sisi tulisahau wajibu wetu wa kuwaweka vizuri. Vibanda kila mahali, hakuna mahali utapita vizuri bila kukuta biashara ya mtu mpaka kwenye mitaro.

“Ukienda shule ya Bunge katikati ya jiji kuna vibanda, IFM vibanda. Nenda daraja la Kijazi watu wanauza supu, miwa, vitunguu… Ni shaghalabaghala. Sasa uongozi ni kutambua tatizo na kurekebisha. Ukijua tatizo usipotatua wewe ni tatizo,” anasema.

Anasisitiza. “Lazima tuweke Dar es Salaam iwe safi na hawa wafanyabiashara ndogondogo wanaojitafutia maisha wawe katika mpangilio. Nendeni nchi yoyote mtaona utaratibu upo. Hapa fanya biashara pale usifanye. Sasa Dar tumeruhusu kila mtu afanye kokote anakotaka. Lazima tujenge heshima ya mji huu ambao ni uso wa nchi unaopokea watu mbalimbali,”.

Anasema tayari kwa kushirikiana na wataalamu ameandaa mpango mzuri wa namna ya kuweka Mkoa wa Dar es Salaam kuwa safi na namna ya kuwapanga wafanyabiashara vizuri.

“Hatuwaondoi ila wapangwe vizuri. Aliyejenga kwenye mfereji au mtaro utauzibuaje asipopangwa vizuri?” Anahoji.

Anasema kuna mahali viongozi hawakutoa mwongozo hivyo atawapa madiwani wa Dar es Salaam mpango wake huo ili wauridhie na kuujadili, waone athari zilizopo kiusalama, kijamii na kiafya kama wafanyabiashara hao wasipopangwa vizuri.

Anasema hata gereji bubu ataziondoa ambazo nazo zipo maeneo mengi mbele za majengo ya watu kiasi cha kuchafua mandhari ya eneo husika.

Anasema atakapozindua mpango wake huo hakuna machinga atakayekosa eneo la kufanya biashara kwani amejipanga vizuri.

Kwa nyakati tofauti katika jiji la Dar es Salaam wafanyabiashara wa nguo, viatu na vyombo katika maeneo ya Kariakoo wamekuwa wakilalamikia wamachinga kwa kupanga biashara zao mbele ya maduka yao ilhali wakiziuza kwa bei ya chini kuliko kwenye maduka.

Wamekuwa wakilalamika kwamba machinga hao hawalipi kodi zaidi ya vitambulisho vya machinga vilivyoanzishwa na serikali ya awamu ya tano, hawalipi kodi ya pango, maji wala umeme na hata gharama za usafi za maeneo yao mara nyingi zinafanywa na wenye maduka.

Hussein Juma, mfanyabiashara wa viatu Kariakoo anasema kuwa kitendo cha wafanyabiashara kuuza bidhaa walizonazo mbele ya maduka yao kunawafanya wateja kuishia kwa machinga bila kufika kwao.

“Hawa machinga wamekuwa wakiuza kwa bei ndogo zaidi tofauti na sisi kwa sababu tunazingatia kodi na tozo mbalimbali tunazolazimika kulipa ambazo wao hawalipi. Wateja wamekuwa wakiishia njiani hawafiki kwenye maduka, kwetu sisi ni hasara,” anasema.

Anapongeza uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuja na wazo la kusafisha jiji na kwamba asisahau kuwasafisha na machinga kwani wanaua biashara zao na kupunguza kodi ya serikali.

“Ninajua machinga wana umuhimu wao, wanajitafutia kipato kwa ajili ya familia zao lakini ni muhimu pia wawe katika maeneo maalumu na siyo kama ilivyo sasa. Mtu anakuja mbele ya duka anafungua biashara yake. Hii haijakaa vizuri kwa kweli,” anasema mfanyabiashara huyo.

Paschal Nyange, anasema amekuwa akifanya biashara ya baba lishe maeneo ya Mnazi Mmoja kwa muda mrefu sasa na kwamba amejijengea wateja wengi.

Licha ya kukiri kwamba anafanyia kazi katika eneo ambalo halijapangwa kwa ajili ya kuuzia chakula lakini anasema uamuzi wa kumhamisha utakuwa na manufaa zaidi kwake kama eneo atakalopelekwa litaleta tija kibiashara.

Naye Mfanyabiashara wa matunda, Tausi Chuma anasema kipato chake kinatokana na matunda anayotembeza pale magari yanapokuwa yamesimama kama ndizi na parachichi.

Anasema endapo watazuiwa kufanya biashara kuna uwezekano mkubwa maisha yake yakawa ni magumu zaidi kwa kuwa haoni sehemu nyingine ambayo itamtoa.

Mfanyabiashara wa nguo za mtumba katika eneo la Kituo cha Daladala Posta Mpya, Joachim Nyee anasema soko lake kubwa limelenga wafanya kazi wa maofisini ambao baada ya kutoka kazini jioni hununua.

“Sikiliza ndugu, unajua nguo hizi za mitumba zinapendwa na wafanyakazi pamoja na wanafunzi wa vyuoni. Sasa ukinitoa hapa utanipoteza katika ramani,” anasema.

Mbaruku Hussein, Msomi wa nadharia mbalimbali za maendeleo anasema nia ya Mkuu wa Mkoa ni njema sana lakini utekelezaji wa mpango wake unapaswa kuzingatia uhusiano wa sekta isiyo rasmi na iliyo rasmi kwamba mara nyingi huwa zinategemeana.

Kwamba sekta isiyo rasmi inategemea kudaka watu walioko ndani ya sekta rasmi na wale wa sekta rasmi pia wakati mwingine huitegemea sekta isiyo rasmi.

“Kwa mfano, nje ya jengo refu la bandari maeneo ya Posta, pale nje utakuta mama lishe wapo. Wako pale ili kudaka watu wanaokwenda kwenye sekta rasmi, yaani kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwenye jengo hilo.

Baadhi yao, wakiwemo wafanyakazi kwenye jengo hilo, hawana uwezo wa kula chakula kwenye hoteli rasmi kutokana na ughali wake na hivyo wanakidhi haja zao za njaa kwa kupata huduma ya mama lishe. Ukiwaondoa pale wale mama lishe na kuwapeleka ambako hakuna sekta rasmi hawatapata wateja na pia watu wanaonufaika na mamam lishe hao utakuwa umewaondolea huduma. Kwa hiyo ni suala la kulingalia kwa umakini,” anasema.