Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 21Article 543616

Habari Kuu of Monday, 21 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ummy atoa siku 2 ma-DC waapishwe

Ummy atoa siku 2 ma-DC waapishwe Ummy atoa siku 2 ma-DC waapishwe

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Makamu wa Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu amewagiza wakuu wa mikoa wawaapishe wakuu wa wilaya leo na kesho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ummy aliwataka wakuu hao wa mikoa waliopo katika majukumu nje ya mikoa yao warudi katika vituo vyao vya kazi kwa ajili ya kukamilisha jukumu hilo haraka iwezekanavyo.

Wakuu hao wa wilaya waliteuliwa Juni 19, 2021 na Rais Samia Suluhu Hassani kushika nafasi hizo.

“Nawataka wakuu wote wa mikoa kuitumia siku ya kesho (leo) kuwaapisha wakuu wa wilaya wote, kusiwepo na visingizo vya aina yoyote kama watashindwa kufanya hivyo Jumatatu basi Jumanne wakamilishe,” alisema.

Ummy aliagiza wateule hao waapishwe haraka ili Jumatano wiki hii waripoti katika vituo vyao vya kazi waanze kutekeleza majukumu yao.

Alimpongeza na kumshukuru Rais Samia kwa uteuzi wa wakuu wa wilaya wakiwemo wanawake 44 ambao ni sawa na asilimia 31.

Alisema kati ya wakuu wa wilaya wote 139 walioteuliwa, 56 ni wapya na 83 wamerejeshwa kwa awamu nyingine wakiwemo 26 waliobakishwa katika wilaya walizokuwa kabla ya uteuzi huo.

“Wengi wamehamishwa ili kwenda kuhamasisha utendaji katika maeneo mapya na wengine wamehamishwa ili kuondoa mazoea waliyokuwa nayo katika vituo vya kazi. Kikubwa nawataka kwenda kufanya kazi kwa kasi, uadilifu, ubunifu na uaminifu mkubwa ili kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Kuhusu wanawake walioteuliwa, Ummy alimshukuru Rais Samia kwa hatua hiyo na kueleza kuwa inazidi kutoa chachu kwa wanawake nchini kuendelea kuchapa kazi, huku akiwataka walioteuliwa kwenda kuonyesha mfano wa utendaji uliotukuka.