Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 25Article 559612

Habari Kuu of Saturday, 25 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Ummy: "ma-DED chanzo wanawake kupigana ofisini"

Ummy: Ummy: "ma-DED chanzo wanawake kupigana ofisini"

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amedai kuwa amebaini kuwapo wakurugenzi wanaume kutumia vyeo kujihusisha kimapenzi na watumishi wa kike.

Amesema tabia ya wakurugenzi hao inasababisha baadhi ya watumioshi kupigana kwa sababu yao.

Aidha, amewapa tumbo joto wakurugenzi wapya 61 wa halmashauri walioteuliwa, hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaambia kuwa wako chini ya uangalizi kwa miezi sita wakipimwa utendaji kazi wao.

Waziri Ummy aliyasema hayo jana kwenye mafunzo elekezi kwa wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa nchini na kusisitiza, kuwa hatavumilia uonevu na udhalilishaji, dhidi ya wanawake kwa kisingizio cha cheo cha ukurugenzi.

“Mimi Waziri ninayemsaidia Rais sitavumilia suala hilo. Sasa  umekuwa mkurugenzi kila mfanyakazi mzuri kwenye halmashauri yako ni wako. hii hapana.

"Hili ni moja ya mada Katibu Mkuu atalisema hapa. Hatuwezi  kwenda hivyo hawa ni binadamu lakini tunazo kesi wakurugenzi wanasababisha watumishi wanawake wanapigana kisa mkurugenzi. Mtu wa aina hii hafai wala hatoshi kuwa mkurugenzi," alisema huku akisema bado hajapata kesi za wakurugenzi wanawake.

"Sijapata kesi za wanawake, lakini wanawake wenzangu twende tukajiheshimu. Hii  ni nafasi kubwa sana, siyo leo upo na huyu, kesho na huyu haileti taswira nzuri kwa kiongozi wa umma katika nafasi," alisema huku akiwataka wakurugenzi wanawake kulinda utu na heshima waliyopewa na rais na kuangalia watu wanaotoka nao kimapenzi.

"Kuna mwingine ametongozwa amekataa basi hapelekwi semina. Anahamishwa kisa amemkataa mkurugenzi. Hebu  tafuta nje ya halmashauri, lakini isiwe chanzo cha wanawake kupigana maana posho nayo huwa kubwa unajengewa nyumba, wanapewa gari inabidi wanawake tu wapigane,"alisema.

Kuhusu wakurugenzi wapya, Waziri Ummy alisema wako chini ya uangalizi kwa miezi sita na wanapaswa kuonyesha uwezo wao, kwenye utendaji kazi kwa kuwa waliteuliwa kwa kuangalia wasifu na utendaji kazi wao, maeneo waliyokuwapo awali.

“Niseme bila kupepesa macho, mpo kwenye uangalizi na tutapima utendaji wenu kwa sababu mliteuliwa kwa kuangalia, CV (wasifu) na utendaji wa huko mlikokuwa. Sasa  kwenye kazi ya ukurugenzi ni watu ambao mtamsaidia Rais Samia kusimamia shughuli za utawala na maendeleo kwenye mamlaka za serikali za mitaa. Hatuwatishi mpo kwenye uangalizi baada ya miezi sita mimi na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu tutapeleka taarifa kwa rais, atafanya uamuzi,” alisema.

Pia aliwataka wakurugenzi wa zamani, ambao wameaminiwa tena kuongeza kasi ya utendaji kazi, huku akisema wengine wamerudi baada ya Rais Samia kuona awape nafasi tena.

“Mheshimiwa rais ameona asihukumu, labda kulikuwa na changamoto, kwa hiyo hii ni second chance, lakini kubwa ni imani kubwa kwa rais kwetu, mafunzo haya ni ya kukumbushana namna ya kutekeleza majukumu yetu kwenye mamlaka za serikali za mitaa,”alisema.

Alisema ni wakati wao kuonesha uwezo wao wa kiutendaji kwa Mamlaka ya uteuzi na watapimwa kwa matokeo ya kazi zao.

Pia alisema amepokea kesi za wakurugenzi kugombana na wenyeviti wao na kuwataka kutumia mafunzo hayo kujiepusha na migongano hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof. Riziki Shemdoe, alisema hadi juzi kuna halmashauri 22, ambazo hesabu zao hazijasomeka, kwenye mfumo wa fedha wa serikali.

Alitaja Halmashauri hizo kuwa ni Jiji la Dar es Salaam, Bahi, Mvomero, Newala, Newala TC, Chalinze, Kibaha, Songea, Madaba, Itilima, Manyoni, Songwe, Muheza, Bumbuli, Kilindi, Kishapu, Msalala, Shinyanga, Kahama na Lushoto.