Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 22Article 573370

Habari Kuu of Monday, 22 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Undani 'Masharti ya hovyo' bandari ya Bagamoyo

Undani Undani

Miaka sita iliyopita, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo nchini ulikuwa ukitajwa kama mmoja wa miradi ya kimkakati yenye fursa kubwa ya kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, miaka miwili iliyopita, upepo ulianza kubadilika. Aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Hayati John Magufuli, alizungumza hadharani kuhusu mradi huo na kusema ulikuwa na "masharti ya hovyo" ambayo serikali isingeweza kuyakubali.

Kauli hiyo kutoka kwa Kiongozi Mkuu wanchi ilizua mkanganyiko miongoni mwa wananchi; wengine wakiamini wale waliosema bandari hiyo ijengwe na wengine wakiamini mradi huo ni wa hovyo.

Hiyo ndiyo Tanzania ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameirithi linapokuja suala la ujenzi wa bandari hiyo. Kwenye kujibu swali kubwa la makala haya, ni muhimu kurudi nyuma kidogo kufahamu kuhusu mradi wenyewe.

Mradi wa bandari ya Bagamoyo

Bandari ya Dar es Salaam ndiyo imekuwa kama lango kuu la kupitishia bidhaa zinazokwenda katika nchi jirani zisizo na bahari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Hata hivyo, ingawa huduma za bandari hiyo zinahitajika sana, bandari ya Dar es Salaam kwa sababu tofauti ikiwamo udogo wa eneo lake na ongezeko la mahitaji ya huduma na teknolojia za kisasa za meli, imeanza kuzidiwa.

Iliyokuwa Mamlaka ya Bandari wakati huo, iliona changamoto hiyo na ndiyo ikapendekeza kujengwa kwa bandari nyingine kubwa zaidi katika eneo la Bagamoyo umbali wa takribani kilomita 75 tu kutoka Dar es Salaam ili kuendelea kuwa kitovu cha usafiri wa maji katika eneo la Afrika.

Katika kutimiza adhma hiyo, Mamlaka ya Bandari ikaja na Mpango Kabambe wa Miaka 20 wa Uendelezwaji wa Bandari za Tanzania ambao pamoja na mambo mengine, ulipendekeza Bandari ya Bagamoyo ijengwe katika miaka ya 2021/2022.

Sababu nyingine ambayo ni ya kijiografia ni kwamba eneo la Bagamoyo ni mojawapo ya maeneo ambayo China imeyatambua kama ya kimkakati katika Mpango wake Kabambe wa Belt and Road ambao kimsingi unaunganisha dunia kupitia njia ya maji.

Tanzania iko katika eneo la kimkakati kwa sababu inazungukwa na nchi nyingi zisizo na bahari, tayari ina reli mbili zinazounganisha na nchi jirani; TAZARA kwa maana ya Zambia na ile ya Kati inayokwenda mpaka Kigoma ambako ni jirani na Congo, Rwanda na Burundi.

Kama ujenzi wa Reli ya Mwendokasi (SGR) ukikamilika, Tanzania itakuwa na reli ya kisasa ya kusafirisha watu na mizigo kutoka Tanzania kwenda katika nchi jirani kwa haraka.

Kwa hiyo, wakati Tanzania ikipanga kuwa na Bandari ya Bagamoyo kubwa na imara, wawekezaji kutoka China na Oman waliona fursa ya Eneo la Uwekezaji wa Biashara (EPZ) katika mji huo kwa sababu ya urahisi wa kusafirisha bidhaa kutoka eneo la Maziwa Makuu kwenda kwingineko duniani.

Faida nyingine ya Bandari ya Bagamoyo ilikuwa kwamba kwa sababu ya ukubwa wake, itakuwa na uwezo wa kupokea mizigo zaidi ya mara 20 ya Bandari ya Dar es Salaam na pia kupokea meli kubwa za kisasa ambao kwa sababu ya ukubwa wake, haziwezi kuja Dar es Salaam.

Kupitia mradi wa EPZ, ilielezwa vitafunguliwa zaidi ya viwanda ya 700 na kuajiri takribani watu 250,000 ukiwamo mradi wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano kutoka kwa wawekezaji kutoka Korea Kusini.

Huu ulikuwa uwe mradi mkubwa zaidi katika historia ya Tanzania ambako wawekezaji hao kutoka China, Oman na Korea Kusini wangeingiza zaidi ya dola bilioni 10 (zaidi ya shilingi trilioni 23).

Wawekezaji hao ni China Merchants Ports Limited(China), Mfuko wa Uwekezaji wa Oman (OIA), na Science and Technology Policy Institute(STEPI)Korea Kusini.

Hofu ya Mradi wa Bagamoyo

Maneno ya Hayati Magufuli yalikuja katika wakati ambao kulikuwa na taarifa nyingi kuhusu namna China inavyotwaa mali zisizohamishika za nchi zilizokopa fedha kutoka kwake na zikashindwa kurejesha kwa wakati. Mifano iliyokuwa ikitolewa sana ilihusu nchi kama Zambia na Sri Lanka.

Katika mkutano wake na wafanyabiashara wa Tanzania, Magufuli alizungumza waziwazi kwamba kwa namna makubaliano yale ya Tanzania na wawekezaji yalivyokuwa, mkataba ule ulikuwa hauna maslahi na Tanzania naye asingekubali kuona mradi huo ukiendelea kwa namna hiyo.

"Yaani kwenye eneo lote kuanzia Tanga hadi Mtwara kusijengwe bandari yoyote. Bandari ya Kilwa tusiiendeleze, Bandari ya Mtwara ambayo itawezesha mikoa ya Kusini kupokea mafuta badala ya Dar es Salaam kisha yarudi huko, hatutakiwi kuiendeleza, barabara kutoka Mtwara hadi Bamba Bay ambayo itatuwezesha kusafirisha mizigo hadi Msumbiji tusiijenge," alisema Rais Magufuli.

Hayati Magufuli alisema masharti mengine ya kufanyika kwa mradi huo ni kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotakiwa kwenda kukusanya ushuru wala kodi katika eneo hilo, umiliki wa eneo hilo kwa miaka 33 na kufidiwa kwa gharama za uwekezaji wa ujenzi huo.

Spika Job Ndungai aliwahi kusema kuwa serikali inafanya makosa kutoendelea na mradi huo kwa vile una faida kubwa na kuwa kasoro hizo zilipo kwenye mikataba zinaweza kuzungumzika.

Kuna ukweli kwenye madai ya "mkataba wa hovyo"?

Mmoja wa viongozi wa juu katika utawala wa Mstaafu Jakaya Kikwete ambao mradi huo ulikuwa unaelekea kukamilika, aliwahi kuiambia BBC Sawahili kuwa mengi ya yanayoyosemwa kuhusu mradi huo hayana ukweli na kwamba kulikuwa na upotoshaji mkubwa.

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yake, kiongozi huyo alisema gharama pekee kubwa ambayo serikali ingetakiwa kuingia katika mradi huo ni ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaohamishwa kupisha ujenzi wa bandari hiyo ambao kwa makisio ya mwaka 2016 yalikuwa kiasi cha dola takribani dola milioni 20.9 (shilingi bilioni 43).

" Gharama yetu ni hizo dola milioni 20 za kulipa wananchi lakini mengine yote ni siasa tu. Wanaokuja wanaleta shilingi trilioni 23 na ni uwekezaji wala si mkopo. Ni sawa na kampuni zinazokuja kuchimba madini hapa kwetu. Huwezi kusema wanakuja kutukopesha hela za kuchimba madini. Ni biashara yao.

" Jambo la muhimu kuliko yote ni kwamba huo mpango wa kuwa na Bandari ya Bagamoyo tulikuwa nao hata kabla wawekezaji hawajaja. Na wala hakuna masharti ya kutuzuia kujenga barabara wala miundombinu mingine. Hilo suala la miaka 33 ni la kawaida, yaani mtu aweke shilingi trilioni 23 na halafu asiweke muda wa kurudisha hela zake? Mwisho kabisa, baada ya miaka 33, bandari na hivyo viwanda havitahamishwa Tanzania na nina imani nchi yetu itakuwepo bado," alisema kiongozi huyo.

Alichofanya Rais Samia

Novemba 17, 2021, Serikali ya Rais Samia ilisema kuwa siku za hivi karibuni itaanza mazungumzo na wawekezaji wa Bandari ya Bagamoyo ili kuendeleza eneo kwa ajili ya kujenga bandari, eneo la viwanda na eneo la masuala ya usafiri na usafirishaji.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, jijini Dar es Salaam.

Mwambe, alisema Kampuni za China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (SGRF) zitazungumza na serikali.

Alisema majadiliano yatahusu uendelezaji wa eneo dogo la hekta 3,000 kati ya hekta zote 9,800 za mradi mzima wa eneo maalumu la kiuchumi Bagamoyo (BSEZ).

Mwambe alisema miradi inayotarajiwa kujengwa kwenye eneo hilo ni pamoja na Bandari ya Bagamoyo, eneo la viwanda na eneo la usafiri na usafirishaji.

“Tumefanya uchambuzi wa nyaraka zote muhimu, kwa hiyo mazungumzo yataanza karibuni kati ya Serikali na zile pande mbili ambazo ni Kampuni za China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA),”alisema Mwambe.

Pia aliwataka watu wanaomiliki maeneo kwa ajili ya kujenga viwanda kwenye eneo la hekta 9,800 wawasiliane na serikali wakionesha kusudio la kujenga viwanda hivyo ili maeneo yao yaingizwe kwenye mpango huo kabambe wa uendelezaji wa eneo hilo.

Mwambe alisema mradi wa Bagamoyo ni wa serikali na kwamba kampuni ya China na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ndiyo waliofanya usanifu (design) na ndiyo watakaojenga na uendeshaji ili warudishe gharama za ujenzi na kisha kuukabidhi kwa serikali.

“Kwa hiyo taasisi hizi mbili ya China na ya Oman watakuja na fedha, teknolojia na menejimenti, na sisi serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) tutaingia pia kwa sababu bandari imelipia fidia lile eneo. Tutakuwa na kampuni ya ubia itakayosimamia mradi ule kati ya taasisi hizi mbili na TPA,”alisema Mwambe.

Mwambe alisema hata madai kwamba Wachina walitaka isiendelezwe bandari yoyote kutoka Mtwara mpaka Tanga si ya kweli bali walichoomba Wachina ni kwamba kutoka Dar es Salaam mpaka Pangani pasiendelezwe bandari kama inayotaka kujengwa Bagamoyo kwa sababu hawatapata faida kutokana na uwekezaji watakaoufanya ambao ni zaidi ya Dola bilioni 10.

Alisema hata madai ya kuwa watauendesha mradi huo kwa miaka 99 si ya kweli ila suala hilo litaamuliwa na mfumo wa hesabu za kiuchumi.