Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540445

xxxxxxxxxxx of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Utafiti wa nguvu kazi, rasilimali watu waja 

KATIKA kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi yanafikiwa, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), imepanga mwaka huu kufanya tafiti mbili kubwa ambazo zitajikita kwenye kubaini nguvu kazi pamoja na rasilimali watu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo juzi jijini hapa.

Jenista alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanaendelea kushirikiana ambako wizara hiyo inapitia sera ya elimu na huku ikifanya tafiti.

“Mwaka huu tumeamua kufanya tafiti mbili kubwa ambapo tafiti moja tunaendelea nayo ambayo ni hali ya nguvu kazi nchini. Utafiti huo utatusaidia kujua ni asilimia ngapi ya vijana wanaofundishwa ndani ya nchi na wanaweza kuajirika nchini na kama hawajaajiriki ni kwa nini. Aidha, utafiti huo utatusaidia kuelewa sekta ipi yenye fursa nyingi kuliko sekta nyingine ya ajira hii itasaidia mafunzo ya ufundi yaendane na mahitaji yetu ya ajira,” alisisitiza.

Aidha, alifafanua kuwa serikali imeshakamilisha utaratibu wa kufanya utafiti wa hali ya rasilimali watu nchini ambao utasaidia kuelewa juu ya Watanzania waliopo nchini na waliopo nje ya nchi kama wanaendana na mahitaji ya ajira kwa sasa.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikisimamia vibali vya ajira kwa wageni, hivyo wataelewa sababu ambazo husababisha wawekezaji kuhitaji kuwaleta watu wao wenye ujuzi ilhali wenye ujuzi wa viwango hivyo wapo nchini, lakini pia itaeleweka maeneo gani ambayo nchi haina ujuzi na wangependa ujuzi huo upatikane hapa nchini.

Aliwataka wadau wa elimu ya ufundi kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha changamoto za ajira zinashughulikiwa ipasavyo. Alisisitiza ili kuwa na uchumi wa kati endelevu hadi kufikia uchumi wa juu kunahitajika kuwa na mfumo rasmi wa kuwandaa vijana katika viwango vya juu vya maarifa, ujuzi, na stadi za kutenda.

Join our Newsletter