Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 05Article 541141

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Utalii waeleza miradi minane ya kimkakati

Utalii waeleza miradi minane ya kimkakati Utalii waeleza miradi minane ya kimkakati

WIZARA ya Maliasili na Utalii katika mwaka wa fedha 2021/2022, imepanga kutekeleza miradi minane ya kimkakati na kimaendeleo ukiwemo wa kuzuia na kupambana na ujangili na biashara haramu ya nyara za serikali.

Akiwasilisha Bajeti ya wizara hiyo, Bungeni Dodoma jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alisema miradi mingine itakayotekelezwa ni wa usimamizi wa maliasili na kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini -(REGROW).

"Pia itatekeleza mradi wa kujenga uwezo wa maeneo ya hifadhi, mapori ya akiba na kikosi dhidi ujangili pamoja na mradi wa kuendelea kupanda miti kibiashara," alisema.

Itatekeleza mradi wa kujenga uwezo wa taasisi za mafunzo ya misitu na ufugaji nyuki na wa kuwezesha tnyororo wa Thamani wa Mazao ya Nyuki (BEVAC) na wa kuongeza thamani kwa mazao ya misitu (FORVAC) na wa uendelezaji wa utalii wa mikutano na matukio (MICE).

Katika kutekeleza miradi minane ya maendeleo, wizara inakadiria kutumia Sh bilioni 152.8 . Miradi hiyo ni ya idara na taasisi za TANAPA, NCAA na TAWA.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 38.9 zitatoka kwa Washirika wa Maendeleo (Fedha za Nje) na Sh bilioni 113.9 zitatoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (Fedha za Ndani), sawa na asilimia 74 ya fedha zote za maendeleo.

Fedha za maendeleo Sh bilioni 152.8 zinajumuisha Sh bilioni 40.1 kwa ajili ya miradi itakayotekelezwa na idara mbalimbali ndani ya wizara na Sh bilioni 112.7 za miradi itakayotekelezwa na taasisi.

Hata hivyo, wizara hiyo imepewa malengo ya kukusanya maduhuli ya serikali ambapo, katika mwaka wa fedha 2021/2022, inakadiriwa kukusanya maduhuli yatokanayo na sekta ya maliasili na utalii ya Sh biliioni 689.34. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 478.01 zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kutokana na vyanzo vya TANAPA, NCAA na TAWA na Sh bilioni 211.3 zitakusanywa kupitia wizara na taasisi zake ikiwemo TFS.

Wizara kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele kwa kuendelea kuimarisha mikakati ya ukusanyaji maduhuli ya Serikali.

Itaendelea pia kuboresha sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia sekta, kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ukiwemo Utalii wa Mikutano na Matukio (MICE tourism).

Hadi sasa sekta ya utalii nchini huchangia wastani wa asilimia 17 ya Pato la Taifa; asilimia 25 ya fedha za kigeni na huzalisha ajira takriban milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.

Join our Newsletter