Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572725

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Utata kauli za viongozi sakata la Umeme na Maji

Utata kauli za viongozi sakata la Umeme na Maji Utata kauli za viongozi sakata la Umeme na Maji

Sakata la uhaba wa huduma ya maji na umeme nchini linachukua taswira mpya kila kukicha, watanzania walio wengi wanategemea kusikia ahueni kuhusu adha hii, lakini kauli za viongozi katika suala hili zinaleta kigugumizi kwani kwani zimeonekana kutofautiana.

Novemba 16, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwa sababu Tanzania ina ardhi, barabara na umeme wa kutosha.

Katika maelezo yake Waziri Mkuu, alisisitiza zaidi kuhusu mazingira rafiki ya uwekazaji nchini na kama inavyojulikana uwekezaji mwingi wa kibiashara unategemea nishati, na kwa taifa kama Tanzania nishati kuu inayotumika ni ya umeme wa maji, na kwasasa taifa linapita katika changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji na umeme, je wawekezaji watakuja kutumia mbadala upi?

"Wawekezaji njooni muwekeze Tanzania, tuna ardhi ya kutosha, umeme, barabara, tuna reli ya kati na tunajenga reli ya kisasa, pia tuna ndege 11 na nyingine zinakuja, tunajenga viwanja ya ndege kila mkoa, hivyo tunauhakika wa usafiri," amesema Waziri Mkuu.

Waziri wa Nishati, January Makamba alinukuliwa akipinga kuwepo kwa mgao wa umeme nchini, kwa kusema kuwa kama Wizara hawatambui juu ya mgao huo ila kinachofanyika hivi sasa ni marekebisho ya mitambo ya kufua umeme.

Ikumbukwe kuwa Novemba 17, 2021 Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, ilitangaza kuhusu kugeukia matumizi ya umeme wa gesi asilia, ambao mchakato wake ulianza miaka ya nyuma kidogo na kusitishwa, mpango huo ulikuwa wa mwaka 2014-2025, ulilenga kutumia gesi asilia ikwemo makaa ya mawe ili kuweza kuzalisha megawati 1583 hadi megawati 10,800 kwa miaka kumi ijayo.

Taarifa hii ya TANESCO inapinga vikali na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati, undani wa sakata hili ni upi? mgao huu wa umeme ni kwasababu ya marekebisho au sababu ya mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha kushuka kwa kima cha maji?

Rais Samia, wakati akishiriki maadhimisho ya jubilee ya miaka 50 ya hospitali ya Bugando, yaliyofanyika jijini Mwanza, Novemba 17, 2021 alikiri kuwepo kwa changamoto ya maji na umeme ambayo aliitaja kusababishwa na vitendo vya ukaidi na makusudi ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakivifanya kwa maslahi yao wenyewe, pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hii ya Rais Samia na Wizara ya Nishati zinathibitisha uwepo wa changamoto hii, lakini pia kauli ya Waziri Mkuu imepangua uwepo wa adha hiyo.

Je, Tanzania ina umeme wa kutosha ama la?