Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 17Article 543025

Habari Kuu of Thursday, 17 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Utatu wa makatibu wakuu na  utoaji wa haki jinai kwa wafungwa

Utatu wa makatibu wakuu na   utoaji wa haki jinai kwa wafungwa Utatu wa makatibu wakuu na  utoaji wa haki jinai kwa wafungwa

“NAWASALIMU kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ndivyo anavyoanza Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, wakati wa mazungumzo yake na wafungwa na mahabusu wa Gereza la Mbozi mkoani Songwe hivi karibuni.

“Kazi iendelee,” wanajibu wafungwa na mahabusu hawa kwa umoja wao. Kwa baadhi yetu tuliokuwa katika msafara ule, tulipigwa butwaa kidogo baada ya kusikia mwitikio ule ‘Kazi Iendelee.”

Kwa hali ya kawaida na katika mazingira yale, ya watu ambao tayari wameshafungwa na wengine ambao ni wengi zaidi hawajui hatima zao, kwamba bado wangeweza kujibu kwa bashasha kubwa ‘Kazi Iendelee’ ilishangaza.

Salamu hii ya Katibu Mkuu aliyoitumia mara kwa mara katika mikutano yake na makatibu wakuu wenzake kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro na Katibu Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk John Jingu, ilianzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Makatibu wakuu hawa katika utatu wao walikuwa katika ziara ya kikazi ya kwanza na ya aina yake ya takribani wiki moja na kila mmoja katika eneo lake, walitatua baadhi ya changamoto walizozikuta katika mikutano yao na watu wa kada mbalimbali.

Profesa Mchome aliyeratibu ziara hii na ambayo madhumuni yake yalikuwa ni kufuatilia na kukagua hali ya utoaji wa haki jinai na haki madai katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi, anasema aliona ni jambo jema kwa makatibu wakuu kuambatana kwa kuwa majukumu yao yalikuwa yanaingiliana mahali fulani.

Hivyo badala ya kila mtu kwenda kivyake vyake, kwenda pamoja kungesaidia kutatua baadhi ya changamoto ambazo pengine isingekuwa rahisi kuzitatua au kuzitafutia ufumbuzi kama kila mmoja angefanya ziara peke yake.

“Wakati nafikiria kuhusu ziara hii ya kufanya tathmini ya myororo wa utoaji wa haki jinai na haki madai katika mikoa hii ambayo tunaweza kusema baadhi ni mipya, lakini pia ipo pembezoni mwa nchi yetu, nilibaini kuwa kuna mambo ambayo ni mtambuka, kuna masuala yanayoihusu utumishi, mengine yanahusu ustawi wa jamii, ya kisheria na yanayohusu Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Kwa hiyo nikawashirikisha wenzangu tufanye ziara ya pamoja ili katika umoja wetu tuifunze, kujielimisha, lakini pia kuzitafutia ufumbuzi changamoto zile ambazo tutaweza kuzitatua pale pale na kwa wakati ule ule na zile ambazo zitahitaji muda zaidi basi kila mmoja atachukua katika eneo lake na kwenda kulifanyia kazi,” anafafanua Profesa Mchome.

Ziara yao ilihusisha kuzungumza na makundi mbalimbali yakiwamo ya vyombo au kamati za utoaji na usimamiaji wa haki jinai na haki madai yaani mahakama, magereza, waendesha mashtaka, Takukuru, ustawi wa jamii na wasaidizi wa kisheria na Jeshi la Polisi. Pia watumishi wa serikali wa halmashauri.

Makubwa yaliyojitokeza katika mikutano hiyo ni changamoto za upungufu wa watumishi, ukosefu wa majengo ya mahakama, magereza; vyombo vinavyohusika kutoa haki kulalamikiwa kujihusisha na rushwa na kusababisha haki ya wananchi kupotea ama kuchelewa na baadhi ya vyombo kuingiliwa na vingine mfano Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) huingiliwa utendaji na watendaji wa serikali.

Nyingine ni baadhi ya watuhumiwa kulalamikia kitendo cha kubambikiziwa kesi na walalamikaji kwa kushirikiana na idara za kutoa haki ambazo hazina uaminifu kwa lengo la kuwakomoa au kulipa kisasi.

Kutofikishwa mahakamani kwa kesi nyingi za mahabusi kwa kigezo cha upelelezi kutokamilika na wafungwa wengi kushindwa kukata rufaa kutokana na kukosa nakala za hukumu au nakala hizo kuchelewa kutolewa.

Nyingine ni kukosekana kwa wakalimani wakati wa kusikiliza kesi au malalamiko yao; masharti magumu ya dhamana na uhaba mkubwa wa maji katika magereza.

Mkoani Songwe, Mahakimu wa Mahakama ya Momba, Ileje na Mbozi walikuwa wa kwanza kuelezea hali ya utoaji wa hakijinai mkoani humo.

Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Momba, Timothy Lyon alieleza kuwa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Momba ni la kupanga na lipo eneo moja na Nyumba ya Kulala Wageni (Lodge).

Aliongeza, “Lakini cha zaidi, lango la kuingia jengo la mahakama na kuingia kwenye nyumba ya wageni ni moja, hali hii si salama sana kwa sababu watu wa aina mbalimbali wanaingia kwa kutumia lango hilo kana kwamba wanakwenda mahakamani kumbe wanakwenda katika nyumba ya wageni. Muingiliano huu si salama na unaathiri shughuli za mahakama na suala utoaji haki.”

Alisema pia kuwa wilaya hiyo haina gereza, inategemea gereza la mkoa ambalo lipo mbali na athari zake ni Pamoja na mahabusu kuchelewa kufika mahakamani na hivyo kesi kuchelewa kuanza.

Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Ileje, Shughuli Mwampashe na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Mbozi, Nemes Chami, walieleza changamoto za ukosefu wa majengo na uhaba wa watumishi.

“Tunazo mahakama za mwanzo tano na mahakimu wawili, hawa wanapotakiwa kwenda nje ya kituo usafiri wanaoutumia ni wa pikipiki na maeneo wanayokwenda ni ya mvua kipindi chote. Lakini anakuwa hakimu yeye, karani yeye na mhudumu yeye, hii inaathiri sana utendaji wa majukumu yetu hivyo tunaomba tuongezewa mahakimu na watumishi wa kada nyingine,” alisema Mwampashe.

Na kama ilivyokuwa kwa Wilaya za Ileje na Momba, Mbozi pia haina gereza, watuhumiwa wake hupelewa gereza la mkoa lenye uwezo wa kuhudumia wafungwa na mahabusu 100. Hata hivyo wakati ziara lilikuwa na wafungwa zaidi ya 400.

Mahakimu hao walizungumzia pia changamoto ya upatikanaji wa maofisa wa ustawi wa jamii hususani kwa kesi zinazowahusu watoto waliokinzana na sheria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Songwe, Wakili wa Serikali Ofmedy Mtenga alizungumzia zaidi kwa nini upelelezi wa kesi unachelewa, malalamiko ambayo yalitolewa na mahakimu. Lalamiko hili lilirudiwa na wafungwa na mahabusu ya Magereza ya Mbozi na Mpanda kupitia risala yao mbele ya makatibu wakuu.

Mtenga anakiri kuna ucheleweshaji mkubwa wa upelelezi kwa kile alichosema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Songwe ina mawakili wa serikali wawili wanaoshughulikia majalada ya kesi za mauaji 120 na kesi nyingine 254. Mzigo mkubwa kwao unaochangia kuchelewesha upepelezi.

Wakiwa Gereza la Mahabusu la Mbozi, walikuta wafungwa na mahabusu wapatao 448 kwa upande wa gereza la wanaume.

“Waheshimiwa makatibu wakuu, sisi (mahabusu na wafungwa) tumefurahishwa sana na ujio wenu, na wewe katibu mkuu wa sheria ndiyo mwenyewe, tunakuomba basi, uangalie uwezekano wa kutungwa kwa sheria ya ukomo wa upelelezi ili haki itendeke mapema, na mtuhumiwa ajue hatima yake kama anafungwa au anaachiwa huru.

“Wengi wetu humu tumeshakaa muda mrefu inauma na inasikitisha sana, na sisi tuna familia zetu, tuna shughuli zetu, tusaidie katika hili,” alisema Ali katika risala yao.

Malalamiko ya kubambikiwa kesi ni moja ya hoja ambayo viongozi hao walikutana nayo katika magereza mawili walioyatembelea na kuzungumza na wafungwa na mahabusu.

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika Gereza la Mpanda, ambapo asilimia 95 ya mahabusu waliokuwapo walikuwa ni watuhumiwa na kesi za mauaji, hali hii iliwashtua kwa kiasi kikubwa kiasi cha kuulizana kulikoni.

“Eeh wote nyinyi mmeua?” alihoji tena Katibu Mkuu huku baadhi yao wakijibu, “tumebambikizwa kesi.”

Katibu Mkuu anatoa nafasi kwa mahabusu watatu waelezee namna walivyobambikizwa kesi hizo.

Mahabusu Mzee Hilary (siyo jina lake halisi) anasimama kwa shida kidogo. Anasema ana miaka 62 na amekuwa katika gereza hilo tangu mwaka 2017 alipokamatwa. Anadai Polisi walimchukulia fedha zake kiasi cha Sh milioni sita na kisha akabambikiwa kesi ya mauaji na tangu wakati huo bado yupo mahabusu na upelelezi haujakamilika.

“Mheshimiwa naomba nikupe makaratasi yangu, mimi nina miaka 62, fedha yangu imechukuliwa, hatima yangu siijui, watoto wangu hawaendi shule…mimi sikusoma, lakini ninataka watoto wangu wasome, basi kama mnataka niendelee kukaa humu ndani nirudishieni fedha yangu tu ili watoto wangu waendelee na masomo. La sivyo basi wachukueni muwasomeshe gawaneni watoto wangu” alisema mzee huyo katika hali ya majonzi makubwa.

Idadi kubwa ya mahabusu wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji katika Gereza la Mpanda ambao kwa wale majalada yao yalikuwa yamefungwa walikuwa 71 na kwa wale ambao mashauri yao upelelezi ulikuwa unaendelea walikuwa 80.

Makatibu wakuu hawa wanaona ipo haja ya kuunda timu maalumu ambayo pamoja na mambo mengine ifuatilie ukweli yalioelezwa.

Pia wanaona kwamba kutokuwapo kwa jaji katika mkoa huo, ni moja ya sababu za mahabusu kuendelea kukaa ndani kusubiri vikao maalumu ambavyo hufanyika mkoani Rukwa. Wanaamini pia kuchelewa huko kunatokana na kesi nyingi kuwa za kubambikizwa.

Kwa msingi huo, waliwaomba makatibu wakuu kutumia vikao vyao na Rais kuomba na kupendekeza Mkoa wa Katavi nao upatiwe jaji ili kasi ya usikilizwaji wa mashauri yao uongezeke na kwa tija inayotakiwa.

Katika ziara hii, pamoja na kufanya tathmini ya mnyororo wa utoaji haki unavyotekelezwa katika mikoa hiyo, ililenga kutoa maelekezo yakiwamo ya utoaji wa adhabu mbadala kwa mashauri yanayoweza kufanyiwa hivyo lakini pia kusisitiza umuhimu wa kutumia njia za majadiliano na makubaliano badala ya kukimbilia mahakamani.

Katibu Mkuu Mchome alieleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ilichukua jitihada za makusudi za kufanya maboresho makubwa katika mfumo wa haki jinai ili kukabiliana na changamoto za ucheleweshaji wa mashauri, mlundikano wa mashauri na msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani na vituo wanamozuiliwa.

“Katika kipindi hiki tumeshuhudia kuboreshwa kwa mfumo wa majadiliano na makubaliano katika makosa ya jinai. Upatanishi katika mkosa ya jinai na ufifishaji wa makosa ya jinai. Na kwenye mfumo wa haki madai yalifanyika marekebisho ya sheria kuboresha utaratibu wa utatuzi wa migogoro mbalimbali kwa njia za upatanishi, majadiliano, maridhiano na usuluhishi,” anaeleza Profesa Mchome.

Anavishauri vyombo vya utoaji wa haki kutumia mabadiliko haya ya sheria kwa mfano ufifishaji wa makosa ambao anasema ni utaratibu uliopo kisheria wa kutoa faini kwa makosa yanayoruhusu faini badala ya kifungo.

“Utaratibu huu uko wa aina mbili; ule wa kimahakama na wa nje ya mahakama kwa kutumia taratibu za kisheria zinazohusu baadhi ya watu/maofisa kufifisha makosa. Kwa hiyo ningependa sana kuwasisitiza kutumia njia hizi za mbadala ili kuharakisha utoaji wa haki kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria.

Mwandishi ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.