Uko hapa: NyumbaniHabari2019 11 15Article 488041

Habari Kuu of Friday, 15 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

VIDEO: Butiku alivyomzungumzia Mwalimu Nyerere mbele ya wasanii wa Tanzania

VIDEO: Butiku alivyomzungumzia Mwalimu Nyerere mbele ya wasanii wa Tanzania play videoVIDEO: Butiku alivyomzungumzia Mwalimu Nyerere mbele ya wasanii wa Tanzania

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi Mwalimu Nyerere nchini Tanzania, Joseph Butiku amemuelezea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama mtu aliyependa na kuijua sanaa.

Butiku ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 15, 2019  wakati wa kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere linalofanyika jijini Dar es Salaam ambalo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Tanzania, John Magufuli.

“Mwalimu  alikuwa gwiji wa sanaa. Alikuwa ni mtu wa imani kwa Mungu wake na imani kwa binadamu wenzake, aliwapenda,” amesema Butiku

Butiku amewakumbusha Watanzania na wasanii kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufuata misingi aliyoisimamia.

“Msingi wa taifa hili haukuanza na azimio, ulianza na nafsi ya mwalimu na katiba ya Chama cha Tanu, binadamu wote ni sawa na sisi ni familia moja.”

“Tuna haki sawa, haki ya Uhuru, haki ya kusema, haki ya kushiriki. Huyo ndiyo Nyerere na hiyo ndiyo Tanzania tusisahau misingi hiyo,” amesema

Butiku amesema, ”Sisi ni watu sawa katika haki zetu zote Tanzania, Afrika na dunia. Msisahau misingi ya Mwalimu itikadi pili vyombo vinavyosimamia itikadi hiyo.”

Kwa upande wake, mwakilishi wa familia ya Nyerere, amemtaja muasisi huyo kama mtu aliyependa sanaa.

“Mwalimu Nyerere alikuwa anapenda taarab wasanii kama Issa Matona walikuwa wanakuja nyumbani kuburudisha kwenye shughuli za kifamilia,”

Mwalimu Julius Kambarage Nyererere aliyezaliwa Aprili 13 mwaka 1922 alifariki dunia Oktoba 14, 1999 London nchini Uingereza alikokwenda kwa matibabu. Mwalimu Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kati ya Oktoba 29 mwaka 1964 hadi Novemba 5 mwaka 1985.