Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 18Article 572335

Habari Kuu of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Vichwa, mabehewa ya treni kuanza kuzalishwa nchini

Vichwa, mabehewa ya treni kuanza kuzalishwa nchini Vichwa, mabehewa ya treni kuanza kuzalishwa nchini

Endapo mipango itatimia kama ilivyopangwa, ndani ya mwaka mmoja ujao Tanzania itaanza uzalishaji wa vichwa vya treni na mabehewa na kuuza nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Hayo yalielezwa jana na Mwakilishi wa Kampuni ya SMH Rail ya Malaysia, Mussa Mansour wakati wa hafla ya kupokea vichwa vitatu vya treni ya aina ya H10 series vinavyotarajia kutumiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mansour alisema kampuni hiyo imekuwa ikifanya ukarabati wa vichwa na mabehewa ya TRC tangu mwaka 2013 na uwekezaji unaotarajiwa kufanyika una thamani ya kati ya dola 40 milioni za Marekani (Sh92 bilioni) hadi dola 100 milioni (Sh230 bilioni).

“Tumepanga kuwekeza ili vichwa vya treni na mabehewa viwe vinatengenezwa hapa, tumelenga soko la EAC na Sadc. Tayari Serikali imetupa ekari 50 huko Kwara, Kibaha tunaendelea na taratibu zetu na huenda tukaanza ujenzi Desemba 15 ambao utachukua si zaidi ya mwaka, ajira zitakazozalishwa ni zaidi ya 1,000,” alisema Manour.

SMH, ambayo makao yake makuu yapo jijini Kuala Lumpur nchini Malaysia inajihusisha na usanifu, uhandisi, uzalishaji na ukarabati wa vichwa vya treni na mabehewa ya Metre Guage na Standard Guage.

Awali, akizungumza baada ya kupokea vichwa hivyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alizungumzia utayari wa Serikali kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho, akisema kitakuwa na manufaa kwa pande zote mbili na bei ya bidhaa husika itapungua tofauti na sasa, jambo ambalo Mansour alikubaliana nalo, licha ya kuwa hakusema ni kwa kiwango gani bei hizo zitapungua.

Profesa Mbarawa alisema Serikali inakusudia kufufua shughuli za treni katika usafirishaji mizigo na abira, akisema lengo siyo wenye malori na mabasi wasipate kazi, bali kuboresha shughuli za uchukuzi na kukuza uchumi wa nchi.

“Tunaendelea kufanya maboresho ya bandari na huduma za treni kwa kuwa zinategemeana, kwa vichwa hivi vitatu na vingine vinavyotarajiwa kutumika katika reli ya kati vitaongeza ufanisi wa TRC na bandari,” alisema Profesa Mbarawa huku akigusia ujenzi wa SGR unaoendelea, akisema juhudi zote hizo zinalenga kuboresha sekta ya uchukuzi nchini.

Aidha, Profesa Mbarawa aliwataka TRC kuwaza kibiashara shughuli zao zote, akisema wanapaswa kununua vifaa vyao kutoka chanzo kimoja ili kupunguza gharama za ukarabati pindi vinapoharibika, kuwa na wataalamu wa kutosha kuvihudumia, urahisi wa bei za vipuri pamoja na kupata waranti ya muda mrefu.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema maboresho yanyofanywa katika shirika hilo yanalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwa miaka miwili hadi mitatu ijayo sekta ya uchukuzi nchini itakuwa imepiga hatua kubwa, huku mchango wake katika pato la Taifa ukiongezeka.

Mbali na ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea hivi sasa, alisema pia kufanya usanifu yakinifu wa madaraja ya reli ya zamani ili kuyafanya yaweze kubeba uzito zaidi, tofauti na sasa ambapo yaliyo mengi yanaweza kupitisha mpaka tani 40 tu kwa ekseli moja.

Akizungumzia ujio wa mabehewa hayo, alisema yalitakiwa kuwasili nchini siku 424 zilizopita, lakini yalichelewa kwa sababu ya mlipuko wa Uviko-19, hata hivyo alisema ni ya kisasa na yana uwezo mkubwa kuliko yaliyopo, hivyo yanakwenda kuongeza ufanisi wa shirika hilo, hususan usafirishaji wa mizigo.

“Vichwa hivi ni rafiki kwa mazingira, kiwango chake cha hewa ya ukaa ni kidogo, vina nguvu ya hourse power 3,000 tofauti na yalivyonavyo sasa ambavyo vina horse power 2,200. Sasa tutabeba mzigo zaidi kwa urahisi,” alisema Kadogosi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula alisema kilichosababisha watu waache kusafirisha mizigo yao kupitia reli ni ufanisi usioridhisha, lakini kwa sasa TRC wanafanya vizuri na inalipa kufanya nao biashara.