Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 584845

Uhalifu & Adhabu of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Vielelezo sare za jeshi vyakataliwa kesi ya Mbowe

Vielelezo sare za jeshi vyakataliwa kesi ya Mbowe Vielelezo sare za jeshi vyakataliwa kesi ya Mbowe

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imekataa kupokea sare za Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na ramani za vituo vya mafuta kama vielelezo vya ushahidi kwenye kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Uamuzi huo ulitolewa jana baada ya kukubaliana na hoja mbili za

mapingamizi ya upande wa utetezi katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Upande wa utetezi ulikuwa ukipinga kupokelewa kwa vielelezo hivyo mahakamani hapo.

Uamuzi huo mdogo katika kesi ya msingi ulitolewa na Jaji Joachim Tiganga baada ya kupitia mapingamizi hayo pamoja na hoja za majibu ya upande wa Jamhuri, ambapo alitupilia mbali hoja nyingine zote na kukubaliana na hoja mbili alizoona zina mashiko.

Hoja hizo ni kutowekwa alama katika sare za jeshi pamoja na kutowasilishwa risiti ya vitu vilivyokamatwa kwa mshtakiwa Khalfan Bwire alipopekuliwa nyumbani kwake.

“Mahakama inaona hoja zote zilizotolewa na upande wa utetezi hazina mashiko isipokuwa hoja mbili ambazo imezikubali, kwamba shahidi hakuwasilisha risiti ya kuonesha vitu mbalimbali alivyokamata na alama iliyowekwa, kwa utambuzi wa sare haikuwa sahihi kwa mujibu wa maelekezo yaliyopo katika muongozo wa Jeshi la Polisi (PGO),” alisema Jaji Tiganga.

Alisema kwa mujibu wa PGO, kielelezo kinapokuwa ni nguo kinapaswa kuwekwa alama kwa kamba ambayo itapita kwenye vishikizo na ining’inie na eneo la kuwekwa alama limeelekezwa.

“Kielelezo ambacho kinatakiwa kuwekwa alama kinatakiwa kubanwa na pini, alama hiyo inatakiwa kuwa na namba, kutokana na maelezo hayo kisheria yaliyoelezwa katika PGO, hiyo ni wazi kuwa alama iliyowekwa siyo ambayo PGO 229 imeitambua na kuelekeza,” alisema.

Mbali ya hoja ya alama katika sare, upande wa utetezi pia uliweka mapingamizi ya kutopokelewa vielelezo hivyo mahakamani kwa kile walichodai kutowasilishwa kwa risiti iliyopaswa kutolewa baada ya ukamataji wa mali husika, ambapo Jaji Tiganga alisema kushindwa kutoa risiti pia kuna athari zake.

“Panapokuwa pamefanyika upekuzi kwenye nyumba, boksi au eneo, ofisa ambaye amekamata mali anatakiwa kutoa risiti kuhusu mali alizokamata, hati ya kukamata mali haiwezi kuwa mbadala wa risiti,” alisema Jaji Tiganga.