Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 02Article 545011

Habari za Afya of Friday, 2 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Vijana kutumia mitandao  kuhamasisha upimaji VVU

Vijana kutumia mitandao   kuhamasisha upimaji VVU Vijana kutumia mitandao  kuhamasisha upimaji VVU

“NILICHOFAHAMU mimi ni kwamba ukimwi unaambukizwa kwa ngono zembe tu. Leo ndio nimepewa elimu ya kina juu ya maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda mtoto, nikagundua yapo mambo mengi ambayo vijana hatuyajui kuhusu virusi vya ukimwi (VVU).”

Hayo ni maneno ya mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kutumia simu janja kupitia mitandao ya kijamii katika kuhamasisha wanajamii kupima afya, Diana Gadson.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na taasisi za dini ya Kiisalam na Kikristo (TIP) yalihusisha vijana wa umri wa kati ya miaka 18 hadi 24 wa wilaya za Ilemelea, Buchosa na Kwimba mkoani Mwanza.

Mbali na mafunzo, vijana hao pia walikabidhiwa simu janja 300 (100 kila wilaya), si tu kwa kuhamasisha wanajamii kupima VVU bali pia kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa wakati.

Kabla ya ugawaji wa simu wanufaika walipatiwa elimu juu VVU na namna bora ya kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia na ujumbe wa kuhamasisha upimaji afya.

Mafunzo hayo ni sehemu ya Mradi wa Boresha unaotekelezwa na TIP kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric Aids Health Care Initiative) linalojishughulisha, pamoja na mambo mengine, na uhamasishaji wa kupima VVU.

Mradi huo ulioanza mwaka 2019 na kutarajiwa kumalizika mwaka huu umelenga zaidi kuhamasisha wanaume na watoto (chini ya miaka 18) kupima VVU.

Mshiriki Diana alipendekeza wadau na serikali kutoa elimu juu ya VVU mashuleni ili vijana wengi waweze kuelimika kwa undani zaidi na kuwa mabalozi bora katika kusambaza elimu kwa wanajamii wengine.

“Naona ni elimu pana ambayo inapaswa kutolewa katika sehemu zote zinazohusisha mikusanyiko ya watu, ikiwemo taasisi za elimu ambako ndipo vijana wengi wa rika letu wanapatikana,” anasema.

Anasisitiza kwamba elimu endelevu kwa vijana ni muhimu kwani ndio kundi lililo hatarini kupata maambukizi kutokana na ukweli kwamba vijana wa umri huo (18-24) wako kwenye hatua ya kuanza mahusiano.

Aliendelea kutoa maoni yake kwamba elimu endelevu ya VVU kwa vijana ni muhimu, akarejea jinsi ambavyo washiriki wengi wa mafunzo hayo walikiri kukosa elimu ya kutosha kwani mambo mengine yalionekana mageni kwao.

“Kwa mfano, mbali na kufundishwa jinsi ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda mtoto, tumefahamu pia jinsi ya kuzuia maambukizi mapya kwa mtu na mwenza wake, hata kama wote wanaishi na VVU,” anasema.

Vilevile washiriki walielimishwa jinsi ambayo mwenza mmojawapo anaweza kuwa na maambukizi lakini asimuambukize mwenzake.

Walielimishwa zaidi kwamba hata kama mtu ana maambukizi, hastahili kufanya ngono zembe ili kuzuia maambukizi mapya kutokana na ukweli kwamba zipo aina nyingi za VVU kwa hiyo mtu ajikinge asipate aina nyingine mpya.

Walipewa pia elimu ya kwamba kila mtu inabidi akijinge kwanza, kisha akapime na kujua hali ya afya yake na atakayegundulika kuwa na maambukizi aanze dawa za kufubaza virus (ARVs) mara moja.

Elimu iliyoonekana kuwa ngeni kwa washiriki wa Warsha hiyo pia ni kwamba matumizi bora ya ARVs yanafubaza virusi, hatua inayopunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa maambukizi.

Mratibu wa Ukimwi wilayani Ilemela, Gasper Lugela, anaunga mkono hoja na kupendekeza kwamba upo umuhimu wa kuwafuata vijana walipo, ikiwemo mashuleni na mikusanyiko mbalimbali ya michezo.

Anasema mradi wa ‘Boresha’ utasaidia katika kuhamasisha kwani mwamko kwa watoto/ vijana bado uko chini.

Anasema angalau wale wa umri wa kati ya miaka 25 na 45 wamekua wakijitajidi kupima ispokua wenye miaka kuanzia 15 hadi 24 mwamko uko chini.

“Mwamko mdogo huenda ni kwasabu wengi wenye umri huo wanakua shuleni ambapo vituo vya kupima ni adimu. Nashauri viwepo vituo mashuleni na mahala pengine ambapo vijana wanakusanyika kwa wingi ikiwemo viwanja vya michezo, na tuwe na utaratibu wa kuwafuata hukohuko,” anasema.

Anashauri pia uwepo wa vituo vya kupima VVU katika hospital za binafsi kama ilivyo kwa zile za serikali ili kuongeza wigo wa upimaji wa VVU na kuchukua tahadhari kulingana na majibu ya vipimo.

Mkurugenzi wa TIP, Saida Mukhi, anaunga mkono hoja ya kuwa na vituo vya kupima VVU katika maeneo mbalimbali, akasema TIP imekua ikianzisha vituo katika nyumba mbalimbali za ibada ili kusogeza huduma zaidi kwa wananchi.

Anafafanua zaidi kwamba mradi wa Boresha ulioanza 2019 na kutarajiwa kuisha mwaka huu umehusisha upimaji wa VVU baada ya tafiti mbalimbali kuonesha muamko mdogo wa wanaume na watoto.

Wanawake wako mistari wa mbele lakini ni muhimu sana mtu na mwenza wake kujua hali ya afya zao ili kuchukua tahadhari ama za kuepuka maambukizi au kufubaza virusi endapo watagundulika kuambukizwa, anasema.

Faida nyingine ya wenza kupima ni kuchukua tahadhari ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuwa na kizazi kisicho na maambukizi.

Anawataka wanufaika wa mafunzo na simu janja kuwashirikisha wazazi ili kuhamasisha watoto wao kupima VVU na hivyo kupanua wigo wa vita ya kupinga maambukizi.

“Kila mtu akijua afya yake atachukua hatua stahiki. Kama ana maambukizi ataanza matumizi ya ARVs kwa wakati na kama yuko salama ataendelea kuchukua tahadhari za kujikinga,” anasitiza.

Akizungumzia suala la ukatili wa kijinsia, Mkurugenzi anasema kila taarifa ya ukatili itakayokua ikitumwa kwenye mitandao ya kijamii itakua imeunganishwa moja kwa moja na taasis husika ikiwemo dawati la jinsia la polis, Ustawi wa jamii, maendeleo ya Jamii, Wizara ya afya, TIP na wengine, kwa hatua za haraka.

Kila mshiriki wa mafunzo atakua akitoa taarifa angalau mbili kila siku za ukatili wa kijinsia na kipaumbele ni ukatili wa kingono.