Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 12Article 562813

Habari Kuu of Tuesday, 12 October 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

"Vijana nguvu kazi ya Taifa kwa 56%" Waziri Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Oktoba 12, 2021 amezindua wiki ya vijana kitaifa, Chato Mkoani Geita ambapo amesema Vijana ndio kundi kubwa kwenye nguvu kazi ya Taifa huku akitolea mfano wa utafiti uliofanyika mwaka 2014 ambao ulionesha Vijana walikua nguvu kazi ya Taifa kwa 56%, asilimia ambayo kwa sasa inaamika kuwa kubwa zaidi huku akiwafananisha Vijana na injini au magurudumu kwenye gari hivyo bila uwepo wao gari haliwezi kusogea.

"Kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi ya Taifa (ILFS) wa mwaka 2014 Nchini Tanzania, vijana walibainika kuwa ndiyo kundi kubwa la nguvu kazi ya Taifa kwa asilimia 56%, kundi lenye uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu, kundi lenye ubunifu, uthubutu, ujuzi na uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja, kwa misingi hiyo, Vijana ni injini kwa maendeleo ya Taifa na kwamba Taifa lisilokuwa na vijana ni sawa na gari lisilokuwa na magurudumu kwa kuwa haliwezi kwenda mbele"

"Serikali kutokana na umuhimu huo imeamua kusisitiza matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenu Vijana kwani ninyi ndio Watumiaji wakubwa na Wahanga wakubwa wa TEHAMA, ni ukweli usiopingika kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii yanayoongeza fursa za ajira, Vijana wengi wamefanikiwa kutokana na matumizi sahihi ya TEHAMA hususan kwa kufanya biashara kwa njia ya mtandao, Vijana wameweza kuanzisha na kuendesha vituo vya huduma za intaneti na pia kuanzisha Wakala wa huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu"

"Niwakumbushe kujiepusha na matumizi yasiyo sahihi kama vile wizi na utapeli wa fedha unaofanywa kwa njia ya mtandao, kujiunga na makundi yasiyofaa, kujiingiza kwenye majukwaa ya uchochezi kati ya Mtu na Mtu, baina ya Watu na Viongozi wao lakini pia Taifa na Taifa, vitendo hivi vinavuruga amani, utulivu na mshikamano wetu kama Taifa, napenda mtumie TEHAMA kujiletea maendeleo binafsi na Taifa, pia tafuteni fursa za kiuchumi kupitia TEHAMA na siyo kufanya mambo yasiyofaa kupitia Mitandao" ——— Waziri Mkuu Majaliwa, Chato leo