Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 10Article 556591

Habari Kuu of Friday, 10 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Vituo vya mafuta vilivyopigwa faini ya Tsh. Bilioni 5.1

NEMC yatoza faini vituo tisa vya mafuta bil 5.1/- NEMC yatoza faini vituo tisa vya mafuta bil 5.1/-

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezitoza faini Sh bilioni 5.15 kampuni tisa zinazofanya biashara ya vituo vya mafuta kwa kosa la kuendesha vituo hivyo bila kusajili na kwa kutofanya tathmini ya athari ya mazingira.

Mtendaji Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka alisema Dar es Salaam jana kuwa, baraza hilo liko kwenye kampeni nchi mzima ya kuvibaini vituo vya mafuta vinavyokiuka sheria na kanuni ya mazingira ya mwaka 2004.

Alisema faini hizo zinatakiwa zilipwe ndani ya siku 14 kuanzia leo na muda huo utakapoisha ambavyo vitakuwa havijalipa vitafungwa.

Alitaja kampuni tisa kubwa zilizotozwa faini ya jumla ya Sh bilioni 5.15 kuwa ni kampuni ya Puma ambayo vituo vyake 22 vimetozwa faini ya Sh bilioni 1.1.

Nyingine ni Total ambayo vituo vyake 16 vimekiuka sheria hiyo ya mazingira na kutozwa faini ya jumla ya Sh milioni 800 na kampuni ya Oilcom vituo vyake 12 vimetozwa faini ya jumla ya Sh milioni 600.

Nyingine ni Oryx vituo vyao 15 vimetozwa jumla ya Sh milioni 750, kampuni ya GBP vituo vyake 10 vimetozwa faini ya jumla ya Sh milioni 500, Gapco vituo vyake nane vimetozwa faini jumla ya Sh milioni 400.

Alisema kampuni ya Ester Oil vituo vyake tisa vimetozwa faini Sh milioni 450, kampuni ya Camel vituo vyake sita vimetozwa faini ya jumla ya Sh milioni 300 na kampuni ya TSN vituo vyake vinne vimetozwa Sh 200.

Alisema mbali na kampuni hizo kufanya makosa hayo, pia zimesababishia serikali hasara ya Sh milioni nne kwa kila kituo, fedha ambazo ni kodi ingekatwa kama vingefanya tathmini ya mazingira na kulipa ada ya kazi hiyo kwa wahusika ambao ni baraza hilo.