Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 17Article 543154

Siasa of Thursday, 17 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Vyama vya siasa waomba kukutana na Rais

Vyama vya siasa waomba kukutana na Rais Vyama vya siasa waomba kukutana na Rais

BAADA ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na makundi kadhaa wakiwemo vijana, wanawake, wazee na wafanyabiashara, makundi mengi nayo yameeleza kuihitaji fursa hiyo ya kukutana naye ili wamweleze matarajio yao.

Akizungumza na HabariLEO jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya alisema hatua ya Rais Samia kukutana na makundi mbalimbali ni mwelekeo mzuri.

Sakaya alisema tangu Samia aingie madarakani amekuwa na kauli za kutia matumaini, kauli za kutaka watu wapate fursa, kuwe na demokrasia ya kutosha na kila kundi liweze kuthaminiwa na kupewa kinachostahili.

“Lazima nikiri kwamba ni mwelekeo mzuri kwake, ujue nchi hii ni kubwa ndiyo maana unaona leo anateua, kesho anatengua, huwezi kumjua kila mtu, tumwombee kwa sababu kuongoza nchi siyo kazi ndogo, ni kazi kubwa,”alisema.

Kwa mujibu wa Sakaya, lengo kubwa la Rais Samia ni kuhakikisha taifa linapiga hatua kwenda mbele kwa sababu taifa siyo mti au ardhi, bali taifa ni watu na ili taifa lipige hatua kwenda mbele ni muhimu kukutana na watu na kujua shida zao na kuziwekea mikakati ya kuzitatua.

Alisema Rais Samia ni kiongozi anayependa nchi iwe na demokrasia na anataka kila mtu ashiriki kwenye ujenzi wa taifa kwa kuwa taifa ni la Watanzania wote.

“Natamani pia akutane na viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwa vyama vya siasa vina mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa hili, wazungumze changamoto zilizopo ili kuona namna ya kuendesha taifa kwa pamoja na taifa liwe na umoja wa kutosha,”alisema.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (Tramepro), Bonaventura Mwalongo, alisema ana imani kuwa Rais Samia ataandika historia mpya ya kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wadau wa tiba asili Tanzania.

Mwalongo alisema hatua ya Rais Samia kukutana na vijana jijini Mwanza na makundi mengine ni uamuzi sahihi wa kujua changamoto zao na kuzifanyia kazi.

“Tunatamani kama atatupa wadau wa tiba asili Tanzania nafasi ya karibu ya kukakutana naye, naamini atatoka na mtazamo mpya ambao hakuutarajia ambao utafanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kiafya. Atapata mtazamo na sura halisi ya huduma ya tiba asili na itachochea mwangwi unaoibua utafiti, uzalishaji wa kiviwanda na kupunguza ombwe la utegemezi wa dawa,”alisema Mwalongo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje (Chadema), alisema ni jambo la busara kubwa kwa Rais Samia kukutana na vijana na makundi mengine kwani lina manufaa kwa taifa.

“Rais Samia amechukua nafasi ambayo hakuna mwanamke aliyewahi kuishika katika Afrika Mashariki, ana wajibu wa kutekeleza wajibu wake kama rais katika nchi, pili ana wajibu wa kututengenezea sisi wanawake mazingira mazuri ili kuondoa mtazamo kwamba mwanamke hawezi kushika cheo kikubwa,”alisema Hanje.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Richard Mbunda, alisema hatua ya Rais Samia kukutana na makundi mbalimbali inalenga kujua maslahi, matatizo na mwelekeo wa makundi hayo ili hata atakapohamasisha masuala ya sera ziendane na mahitaji ya makundi hayo ya kijamii.