Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 21Article 558844

Habari za Mikoani of Tuesday, 21 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Vyuo vya ualimu vyaagizwa kutumia Tehama kufundisha

Vifaa vya Tehama Vifaa vya Tehama

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amewaagiza wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu vya umma kutumia Tehama kufundisha ili kuendana na ukuaji wa matumizi ya teknolojia duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 21, 2021 na kitengo cha mawasiliano ya wizara hiyo, Profesa Carolyne ametoa maagizo hayo alipotembelea Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo Tukuyu mkoani humo.

Amesema ni muhimu kwa wakufunzi kuhakikisha wanatumia vema vifaa vya Tehama katika ufundishaji na ujifunzaji ili kuendana na kasi ya ukuaji wa matumizi ya teknolojia duniani hasa katika sekta ya elimu.

Amesema shule nyingi zina vifaa vya Tehama na hata maktaba mtandao hivyo ni vema walimu tarajali wanaotoka katika Vyuo vya Ualimu wakiwa na ujuzi huo watakaoutumia kufundishia wanafunzi wao.

Naye Mkuu wa Chuo, Stephen Mgimba amesema chuo hicho kinatoa mafunzo ya ualimu wa elimu ya msingi, elimu ya awali na stashahada ya elimu ya ualimu wa Sekondari na kwamba kina jumla ya wanafunzi 554.