Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 15Article 551569

Siasa of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

WABUNGE WAWEKEWA UTARATIBU WA CHANJO YA CORONA KWA HIARI

WABUNGE WAWEKEWA UTARATIBU WA CHANJO YA CORONA KWA HIARI WABUNGE WAWEKEWA UTARATIBU WA CHANJO YA CORONA KWA HIARI

OFISI ya Bunge imeandaa utaratibu utakaowezesha wabunge kupata chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 kwa hiari yao katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge ambayo pia ililenga kutoa ufafanuzi juu ya upotoshaji uliofanyika kwenye mitandao ya kijamii.

Upotoshaji huo ni uliodai kwamba, wabunge ambao hawatachanjwa chanjo ya Covid-19, hawataruhusiwa kuingia bungeni.

“Tunapenda kuuulisha umma kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote kwani maelekezo yaliyopo ambayo Spika wa Bunge, Job Ndugai amekuwa akisisitiza ni kuwahimiza waheshimiwa wabunge kujitokeza kuchanja chanjo hiyo kwa hiari yao,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesisitiza wabunge kutumia hiari hiyo kujitokeza kupata chanjo kwa ajili ya kujikinga na kuwakinga wengine.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua utoaji wa chanjo hizo Julai 28 mwaka huu Ikulu Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, hivi karibuni alisema hadi Agosti 4 mwaka huu, jumla ya dozi 1,008,400 za chanjo zilikuwa zimesambazwa kwenye mikoa yote 26 na vituo zaidi 550.