Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 09Article 541885

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

WB kuisaidia Tanzania kukabili athari za corona

WB kuisaidia Tanzania kukabili athari za corona WB kuisaidia Tanzania kukabili athari za corona

BENKI ya Dunia (WB) imefungua dirisha kwa Tanzania la kusaidia kukabiliana na athari za ugonjwa wa Covid-19 katika sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii, biashara na Bajeti ya Serikali.

Hayo yamebainishwa jijini hapa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeziwakilisha Nchi za Kundi la Kwanza la Afrika, Dk. Taufila Nyamadzabo.

Dk Mwigulu alisema ugonjwa wa Covid-19 umekuwa na athari katika Bajeti ya Serikali kwa ujumla, kwa kuwa, kunapotokea changamoto za kiuchumi katika nchi zinazofanya biashara na Tanzania, huathiri makusanyo ya kodi zinazotokana na uagizwaji na uingizaji wa bidhaa na mapato yatokanayo na ufanyaji wa biashara na nchi nyingine.

“Licha ya ahadi ya Benki ya Dunia kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na athari za Covid-19, benki hiyo imeahidi kufungua miradi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ukiwemo mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu ya sekondari nchini, jambo ambalo ni la faraja kwa Taifa kwa kuwa ni eneo ambalo tunalipa kipaumbele,” alieleza.

Aidha, alieleza kuwa mambo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kuwa kati ya asilimia tatu hadi tano, Deni la Taifa ambalo ni himilivu ambalo deni la serikali kwa uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 27.9, ilhali ukomo ni asilimia 70 kwa kutumia vigezo vya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na WB pamoja na mchango wa Benki ya Dunia katika kuweizesha sekta binafsi nchini.

Pia ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kwa kuidhinisha mikopo minne ya masharti nafuu yenye jumla ya dola za Marekani bilioni 1.017 (Sh trilioni 2.3) kwa Serikali ya Tanzania za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ya kuboresha miundombinu ya barabara, kuimarisha mazingira ya ufundishaji na mafunzo katika taasisi za elimu ya juu, kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma bora za umeme visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji, Dk Nyamadzabo aliipongeza serikali kwa jitihada zake za maendeleo na kupunguza umaskini.

Pia alisema serikali inatakiwa kuendelea kukusanya rasilimali kwa ajiri ya kukabiliana na athari za Covid-19 na pia kutumia rasilimali hizo kikamilifu katika kutekeleza miradi ikiwemo inayotolewa fedha na WB na kuishirikisha sekta binafsi katika miradi ya maendeleo ili kuajiri vijana wengi zaidi.

Ameahidi ataendelea kusimama kwa niaba ya Serikali ya Tanzania katika kuiwakilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa WB ili kunufaika kwa ushirika wake na benki hususan katika uidhinishaji wa fedha za miradi ya maendeleo.

Join our Newsletter