Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 07Article 541357

Habari Kuu of Monday, 7 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

WB yaipa fedha zaidi Tanzania

WB yaipa fedha zaidi Tanzania WB yaipa fedha zaidi Tanzania

BENKI ya Dunia (WB) imezidi kuonesha kuridhishwa kwake na Serikali ya Tanzania kwa kuzidi kuipatia mikopo yenye masharti nafuu.

Juni 3, mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi ya WB iliidhinisha mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 142 sawa na Sh bilioni 326.6 kwa Serikali ya Tanzania.

Kwa mujbu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, fedha hizo ni kwa ajili ya mradi wa kuongeza wigo wa huduma bora za umeme Zanzibar (ZESTA).

Alisema awali, Mei 27 mwaka huu, bodi hiyo iliidhinisha mikopo ya miradi mitatu yenye thamani ya Dola milioni 875 sawa na Sh trilioni 2.0125.

Kwa kuzingatia hilo Benki ya Dunia imeidhinisha mikopo ya miradi minne yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.017 sawa na Sh trilioni 2.3391.

Dk Mwigulu alisema mradi wa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma bora za umeme visiwani Zanzibar utasaidia upatikanaji wa huduma bora na za uhakika za umeme visiwani humo.

Alisema hii ni pamoja na kujenga mitambo yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kiwango cha MW 18 kupitia nishati jadidifu ya nguvu ya jua na msongo wa kV132 wa kusafirishia umeme katika visiwa hivyo.

Kuhusu mikopo mitatu ya awali, Benki ya Dunia ilieleza kuwa, kupitia uwezeshaji huo, vyuo zaidi ya 14 nchini vitanufaika, wananchi zaidi ya 35,000 wakiwamo wanawake na vijana watajengewa uwezo na kushiriki kufanya kazi katika miradi ya barabara, na mifumo ya intaneti itaboreshwa kwa kiwango cha juu ili kuongeza kasi ya serikali kutoa huduma.

Tarifa ya benki kwa vyombo vya habari ilisema imeridhia fedha hizo kwa Tanzania kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (IDA) na zimelenga kuongeza kasi ya huduma na wigo wa fursa kwa wananchi hasa wanawake na vijana.

Dk Mwigula alitaja miradi mingine iliyopata idhini ya bodi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa kuboresha barabara za vijijini (RISE) wenye mkopo wa Dola za Marekani milioni 300 na mradi wa kuimarisha mazingira ya ufundishaji na mafunzo katika taasisi za elimu ya juu (HEET) wenye mkopo wa Dola za Marekani milioni 425.

Aliitaja mradi mwingine kuwa ni wa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao (DTP) wenye mkopo wa Dola za Marekani milioni 150.

"Mradi wa Rise utasaidia kuboresha barabara za vijijini na kutoa fursa za ajira takribani 35,000 kwa wananchi wakiopo katika vijiji nufaika pamoja na kujenga uwezo wa usimamizi endelevu wa barabara za vijijini kwa kuhusisha njia shirikishi za jamii,” alisema Dk Mwigulu.

Akaongeza: "Mradi huu utahusisha ujenzi wa kilometa 535 kwa kiwango cha lami katika wilaya sita za mikoa ya Iringa, Lindi, Geita na Tanga na ukarabati wa maeneo korofi ya barabara za vijijini nchi nzima."

Dk Mwigulu alisema mradi wa Heet utasaidia kuimarisha mazingira ya ufundishaji wa mafunzo katika taasisi za elimu ya juu katika fani za kipaumbele cha Taifa kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, kupitia upya na kuboresha mitaala ya vyuo vikuu, kuwajengea uwezo wahadhiri na watumishi wengine ili kuimarisha elimu ya juu.

"Utekelezaji wa mradi huo utawezesha kuwa na wahitimu wanaoendana na soko la ajira na kuchangia maendeleo ya nchi na uchumi kwa jumla," alisema.

Kwa mujibu wa Mwigulu, mradi wa DTP utasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao na kuboresha huduma kwa umma kidigiti kwa Watanzania wote.

Kuhusu deni la taifa, Mwigulu alisema hadi sasa ni Dola za Marekani milioni 26,416.8 (sawa na Sh bilioni 60.719.01) ikijumuisha deni la nje la Dola za Marekani milioni 18,907.7 na deni la ndani ni Dola za Marekani milioni 7,509.1 (sawa na Sh bilioni 17,259.9.

Alisisitiza kuwa, deni hilo ni himilivu.

Alisema makusanyo ya mapato ya serikali yanaendelea vizuri na kwamba, lengo la makusanyo kwa miezi mitatu ya Februari 2021 hadi Aprili mwaka huu, limefikiwa zaidi ya asilimia 82.

Kuhusu akiba ya fedha za kigeni, Mwigulu alisema hadi Aprili 30 mwaka huu ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,969.7 na kwamba, inatosha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 5.8 kiasi ambacho ni zaidi ya lengo

Join our Newsletter