Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 07Article 583996

Muziki of Friday, 7 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Wabongo Kumshuhudia D’Banj Dubai

D'Banj D'Banj

WATANZANIA wameanza kuchomoza katika shindano la kuwania tiketi za bure kuelekea nchini Dubai kutembelea maonesho ya kibiashara ‘Dubai Expo 2020’, kushiriki tamasha maarufu la muziki la ‘Afrobeat zone soundoff’ pamoja na kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo nchini humo.

Tanzania ambayo itatoa washindi watano kati ya 70 watakaopata fursa hiyo, pia washiriki wake watajifunza namna ya kuendesha biashara hiyo ya utalii na kubadilishana uzoefu hasa ikizingatiwa Dubai ni mojawapo ya majiji bora ya kitalii duniani.

Taarifa ya iliyotolewa wiki hii kwa vyombo vya habari na Idara ya Uchumi na Utalii Dubai (DET) ambayo ndio waandaaji wa tamasha na maonesho hayo, inaeleza kuwa hadi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi tisa ambazo washindi wake wameanza kujishindia tiketi hizo.

Washindi wa awali wameibuka kutoka nchi za Marekani, Nigeria, Kenya, Ghana, Zambia, Uganda, Uingereza na Angola ambazo ni kati ya nchi 14 ambazo kila moja itatoa washindi watano watakaojishindia tiketi hizo.

Zaidi ya nafasi 70 za bure zimetolewa kwa mashabiki wenye bahati kwenda kushuhudia tamasha hilo na kujionea vivutio vya utalii.

Akizungumzia tamasha hilo, nyota wa muziki raia wa Nigeria, Oladapo Oyebanjo maarufu kwa jina la kisanii kama D’banj ambaye pia ni balozi wa tamasha la hilo la Afrobeat zone soundoff, amesema lina fursa nyingi na za kipekee.

D’banj ametolea mfano kuwa katika ziara yake ya kwanza, alikutana na mshauri wa nyota kutoka Marekani, Kanye West na sasa mambo yanazidi kumwendea vizuri.

Amesema mashabiki watakaoshinda katika bahati nasibu hiyo wataambatana na watangazaji wa redio nchini mwao ambao wameteuliwa na kufadhiliwa na Idara ya Uchumi na Utalii ya Dubai (DET).

Washindi hao wanaotarajiwa kuelekea Dubai Machi mwaka huu, watapata fursa ya kusafiri na mwenzi mmoja kwani watapata tiketi mbili za kwenda na kurudi, malazi, tiketi ya kuingia kwenye maonyesho ya 2020, na kuingia katika tamasha la kipekee la Afrobeat Desert Safari Party na shughuli zote zinazohusiana na Soundoff.

Mkali huyo wa Afrobeat, D’Banj, ambaye alikuwa msanii wa kwanza wimbo wake wa ‘Oliver Twist’ wenye mahadhi ya Afrobeat kuingia katika chati za nyimbo 10 bora Uingereza, ameahidi wageni watakaohudhuria sherehe hizo kuwapa burudani ya kukata na shoka kupitia uzoefu wake katika tasnia ya muziki aliyonayo.

Katika tamasha hilo la Soundoff ambalo linatarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 9 Machi 2022, D’ banj ameahidi kushusha mvua ya burudani hasa ikizingatiwa watu wengi wataingia katika tamasha hilo ambalo viingilio vyakevimepunguza.