Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 16Article 542986

Habari Kuu of Wednesday, 16 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wabunge wampongeza Rais kwa bajeti inayogusa watu

WABUNGE wametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa amesikia kilio cha wananchi kwa serikali kuja na bajeti ambayo inakugusa maisha yao hasa kwenye sekta za maji, afya, elimu na miundombinu.

Wabunge walitoa pongezi hizo wakati wakichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022, bungeni jana.

Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM) alipiga magoti kuonesha ishara ya kumshukuru Rais Samia kwa bajeti hiyo ambayo aliita ya kipekee kutokana na kugusa Watanzania wote.

"Nimetumwa na wananchi wa jimboni kuja kupiga magoti kuishukuru serikali chini ya Mama Samia kwa kuwa kila Mbunge alikuwa anazungumzia Tarura (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini) kuongezewa fedha miaka mingi lakini tabia ya akinamama hata kama ana homa amelala kitandani mtoto akilia ananyanyuka kumwangalia.”

“Wabunge tumelia sana, mama ana kazi nyingi lakini amenyanyuka na kutoa Sh milioni 500 kila jimbo kwa ajili ya ujenzi wa barabara, jambo hili limegusa wananchi wakafanya sherehe siku tatu sababu ya barabara," alisema.

Kilango alisema kinachotakiwa sasa ni usimamizi wa utekelezaji na kuwasihi mameneja wa Tarura wa wilaya kuhakikisha fedha hizo hazipotei ili matumizi yaonekane kwani endapo zitaibiwa watamuumiza Rais.

Mbunge wa Bahi, Keneth Nollo (CCM) alisema Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Rais Samia si wa kufanyiwa mashinikizo kwa kuwa yupo kwenye chama imara huku akimtaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuacha kushindana naye.

Mbunge huyo aliwahakikishia Watanzania kuwa Rais Samia ana rejea kubwa ya uongozi na kwamba hakuna shaka ya kuwa na wasiwasi kwamba hatalivusha taifa, bali atafanya vizuri zaidi kwa sababu ana msingi mkubwa ambao umetengenezwa na CCM.

"Alinza tangu enzi za Mkapa (Benjamin, Rais wa awamu ya tatu) akaondoka yeye bado ni mwenyekiti (Mbowe), akaja mzee Kikwete (Jakaya, Rais wa awamu ya nne) bado mwenyekiti, akaja Magufuli (John, Rais wa awamu ya tano) yeye bado mwenyekiti, sasa Rais Samia yeye bado mwenyekiti, sasa mtu ambaye amekosa pumzi kabisa amechoka hoi bin taabani anataka kuja kupambana na mwenyekiti mpya.”

"Lakini ukiangalia mwenyekiti wetu ameonesha ni mtu anayejua dunia inavyoenda, ninyi mmeshuhudia hata mitazamo yake, juzi amesema kwamba sasa taifa letu liangalie kuna maendeleo makubwa ya kidigitali yanatokea na akashauri tukifanya namna hii tunaweza kuendelea," alisema.