Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 18Article 543280

Habari Kuu of Friday, 18 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wabunge wapongeza serikali kuhusu posho za madiwani

Bungeni Tanzania Bungeni Tanzania

WABUNGE wameipongeza serikali kwa kuuamua kuwalipa madiwani posho kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali badala ya utaratibu wa zamani ambapo walikuwa wakilipwa na halmashauri zao, lakini wakaomba serikali iongeze kiwango cha posho kutoka Sh 100,000 za sasa kwani hazitoshi.

Jana wabunge waliendelea kuchangia Bajeti ya Kuu ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba bungeni Dodoma wiki iliyopita.

Katika uchangiaji wao jana, wabunge walipongeza serikali kuu kwa kuamua kuchukua mzigo kutoka halmashauri, lakini wakasema posho hiyo haitoshi.

Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni (CCM) alipongeza serikali kuamua kuwapa posho madiwani, lakini akasema hazilingani na kazi nzuri wanazofanya katika kata.

Mageni alisema madiwani ni wabunge wa kata wanaofanya kazi nyingi zikiwemo za kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali katika maeneo wanayofanyia kazi, hivyo waongezewe posho.

"Tumeongeza kwa watendaji, lakini tumesahau kuwaongeza posho madiwani, kuongeza posho kwa diwani ni kuongeza posho kwa jamii anayoisaidia katika eneo lake, hivyo naishauri serikali kuangalia kwa jicho la pili," alisema.

Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM) alisema madiwani na udiwani wenyewe ni kama wabunge katika kata mbalimbali nchini.

Alipongeza serikali kwa kuwalipa posho kutoka mfuko mkuu (Hazina) badala ya kutegemea halmashauri na kuwafanya wawe wanyonge, lakini akashauri iwaongezee kiwango cha posho.

Chikota alisema kuwaongezea posho kutawaondolea unyonge kwa wakurugenzi na hivyo, wanaweza kuhoji mapato na matumizi katika halmashauri.

Kwa mujibu wa Chikota, madiwani wanatakiwa kuwa na uwezo wa kifedha katika maeneo yao ili kutotegemea wakuu wa idara.

Aidha, alisema madiwani pia wanapaswa wasiwe ombaomba ili wawe na uwezo wa kuhoji mapato na matumizi katika halmashauri zao na hata kuwasimamia wakurugenzi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Zuena Bushiri (CCM) alisema madiwani wana kazi nyingi katika kata zao na wawakilishi ambao wanafanya kazi katika maeneo yao.

Wakati akiwasilisha Bajeti Juni 10, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema: "Madiwani ni wabunge wakazi wa kwenye kata zetu ambao kila siku wako na wananchi wetu kwenye kusimamia shughuli za maendeleo.”

“Hata hivyo, katika baadhi ya halmashauri madiwani wamekuwa wakikopwa posho zao, wengine hufikia hatua ya kupiga magoti kwa wakurugenzi watendaji ili walipwe,

Hali hii imekuwa ikipunguza ufanisi katika halmashauri zetu kwa madiwani wengi kufanya maamuzi yanayopendekezwa na wakurugenzi watendaji hata kama hayana maslahi kwa taifa ili waweze kulipwa posho zao.”

Dk Mwigulu akasema: “Napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, serikali kuu ianze kulipa posho za kila mwezi za waheshimiwa madiwani moja kwa moja tena kwenye akaunti zao kwa halmashauri zote zenye uwezo mdogo kimapato."

Alisema halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa wa kimapato (Daraja A) zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za madiwani kupitia kwenye akaunti zao.