Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 12Article 585283

Habari Kuu of Wednesday, 12 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Wadau Wamkumbusha Nape Magazeti Yaliyofungiwa

Nape Nnauye Nape Nnauye

WADAU wa habari nchini Tanzania, wamesema uteuzi wa Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wameupokea kwa matumaini huku wakimtaka afungulie magazeti yaliyofungiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Wakizungumza na wengine kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa nyakati tofauti juzi Jumatatu tarehe 10 Januari 2022, wadau hao likiwamo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na wengine, walisema wana imani na Nape, kwa kuwa aliwahi kuhudumu katika sekta hiyo.

Taarifa ya TEF iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Deodatus Balile, ilisema: “Tunamkaribisha Nape katika Wizara hii na tunaamini atatusaidia kusukuma kwa kasi mchakato wa kufungulia magazeti ya Mawio, Mwanahalisi na Tanzania Daima.”

Ilimwomba pia Nape kutoa msukumo wa mchakato wa kubadili sheria zinazosimamia taaluma ya habari kwa nia ya kukuza uhuru wa vyombo vya habari nchini.

TEF katika taarifa yake ilisema imepokea uteuzi huo kwa matumaini makubwa na inaamini Waziri Nape ataifanyia mema tasnia hiyo.

Aidha, TEF ilimshukuru na kumpongeza aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ashatu Kijaji kwa kufanya naye kazi kwa karibu ikiamini kuwa alikopelekwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, ataendelea kufanya vizuri.

“Tunampongeza aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Dk Jim Yonaz kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. “Tumefanya naye kazi vizuri na kwa ukaribu katika mchakato wa kurekebisha sheria za habari, na sasa tunaamini mchakato huu unaendelea kuwa katika mikono salama,” ilisema taarifa ya TEF.

Aidha, TEF ilimpongeza Mohamed Hamis kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Pia, Dk Zainab Chaula, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, alisema uteuzi huo wa Waziri Nape unapaswa kufungua ukurasa mpya kwenye sekta ya habari ambayo imepitia wakati mgumu kwa miaka ya hivi karibuni.

Msuya alisema tasnia ya habari ni muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo, ila bado ina changamoto kama waandishi kupewa mikataba, malipo kidogo kwa wenye ajira, mazingira magumu ya kufanyia kazi na nyingine, hivyo ni vema Waziri huyo akaanza kuzitatua kwa kushirikiana na wadau.

“Sisi JOWUTA tunampongeza Waziri Nape kupata nafasi ya kurejea katika sekta hii, ni imani yetu alishaanza kutambua changamoto, hivyo ni vema akaanza kuzitatua hasa hili la sheria ya habari na mengine,” alisema.

Nawashukuru sana TEF kwa salaam zenu. NIWAHIKIKISHIE Uhuru wa Vyombo vya Habari uko salama mikononi mwa Mhe. Rais Samia. Na Mimi Kama mwakilishi wake kwenye Wizara hii tutafanya kazi pamoja kufikia matarajio ya WADAU! Tushirikiane kufikia malengo!???????????????? pic.twitter.com/fbiI4m99MF

— Nape Moses Nnauye (@Nnauye_Nape) January 10, 2022

Mhariri Mwandamizi, Jesse Kwayu aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Nampongeza Nape kwa kuteuliwa tena kuwa Waziri mwenye dhamana wa sekta ya habari.

“Ni imani yangu kuwa akiwa nje ya Baraza amesikia kilio kikubwa cha wanahabari kuhusu Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016). Wadau tunaomba marekebisho ya sheria hii. Karibu tuyajenge upya,” aliandika.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Nape aliweka taarifa ya TEF kisha akaandika, “nawashukuru sana TEF kwa salaam zenu. Niwahakikishie uhuru wa vyombo vya habari uko salama mikononi mwa Mhe. Rais Samia. Na Mimi Kama mwakilishi wake kwenye Wizara hii tutafanya kazi pamoja kufikia matarajio ya wadau! Tushirikiane kufikia malengo!”